• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 AM
TAHARIRI: Serikali iingilie kati na kumaliza uhaba wa mafuta unaoshuhudiwa nchini

TAHARIRI: Serikali iingilie kati na kumaliza uhaba wa mafuta unaoshuhudiwa nchini

NA MHARIRI

UHABA wa mafuta unaoshuhudiwa sasa nchini ni jambo linalofaa kutatuliwa kwa haraka.

Ingawa tatizo hili ni la kimataifa, kuna njia ambazo serikali inaweza kutumia kulimaliza, na kuhakikisha wananchi wanapata bishaa za mafuta kwa bei nzuri.

Baadhi ya watu serikalini wanaweza kutoa hoja kwamba hata Nigeria, nchi inayoongoza kwa uzalishaji mafuta barani Afrika, inakumbwa na uhaba huu. Hata kama huo ni ukweli, kiini cha uhaba wa mafuta na kupanda kwa bei kinajulikana.

Kuwekewa vikwazo Urusi (moja ya nchi tatu kuu duniani kwa uzalisahaji mafuta) ni kisingizio tu.

Bei ya mafuta Kenya inapanda kwa sababu tunanunua mafuta ambayo yamesafishwa tayari.

Miaka michache iliyopita, tulikuwa na kiwanda chetu cha kusafirishia mafuta. Kenya Petroleum Refinery Limited (KPRL), kilijengwa na kampuni mbili za mafuta mwaka 1960.

Kampuni ya Shell na British Petroleum (BP), zilijenga kiwanda hicho ili kusaidia eneo la Afrika Mashariki kupata mafuta kwa bei rahisi.

Lakini serikali yetu kupitia ushauri wa watu wanaopenda kuvuna wasipopanda, ikakifunga kwa madai kuwa hakiwezi kuwa na faida tena. Swali ambalo Mkenya aliyekuwa akinunua mafuta kwa bei ya chini atajiuliza ni hili; kiwanda hicho hakikuwa na faida kwa nani hasa? Kwani kumuuzia mwananchi mafuta kwa bei nafuu na kupunguza gharama ya maisha ni hasara?

Serikali huundwa sio kwa faida ya viongozi, bali kutoa huduma kwa wananchi. Kama KPRL ilikuwa inamwezesha mwananchi kupata bidhaa madukani kwa bei nafuu kwa sababu mafuta yalikuwa yakisafishiwa Changamwe, Mombasa, ina maana ilikuwa ikitoa huduma ipaswavyo.

Tatizo la uhaba wa sasa pia kwa kiwango kikubwa linachangiwa na tabia ya serikali kutotekeleza ahadi zake. Miezi michache iliyopita, serikali iliwataka wenye vituo vya mafuta wasiongeze bei, kwa ahadi kuwa ingewapa pesa za kusimamia gharama hiyo. Wenye mafuta wanasema kufikia sasa hawajalipwa na huenda uhaba huu ni ‘mgomo baridi.’

Mafuta ni kiungo muhimu cha uchumi wa nchi yoyote. Bila mafuta, hakutakuwa na uchukuzi. Magari yatakwama, garimoshi, viwanda na hata shughuli nyingi za serikali zitaathirika.

Serikali juzi ililipa na kupunguza bei ya mbolea kwa karibu nusu. Mbolea ni muhimu lakini kukikosekana mafuta kujaza tingatinga na mashine nyingine zinazotumika shambani, itakuwa kazi bura.

Jambo la msingi kwa sasa ni kutimiza ahadi hiyo ya kulipa wasambazaji mafuta, ili athari za uvamizi wa Urusi nchini Ukraine zisilemaze shughuli zetu muhimu.

You can share this post!

Simu za Sudi, Kositany zatwaliwa na DCI baada ya kuhojiwa...

Uteuzi Ukambani sasa wamnyima Kalonzo usingizi

T L