• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
TAHARIRI: Serikali iwaachie maseneta kazi ya kufuatilia pesa zipewazo kaunti

TAHARIRI: Serikali iwaachie maseneta kazi ya kufuatilia pesa zipewazo kaunti

NA MHARIRI

MZOZO unaoendelea kuhusu mwenye mamalak aya kusimamia pesa zinazotumwa kwa kaunti haufai.

Bunge la Kitaifa na lile la seneti, yanaendelea kuvutana kuhusu mwenye jukumu la kufuatilia matumizi ya pesa zinazotolewa kwa masharti. Pesa hizo huwa mara nyingi zinatolewa na wafadhili, kwa lengo la kutimiza mahitaji maalumu.

Kwa mfano katika kaunti kama ya Uasin Gishu, wafadhili huenda wakataka kuipa serikali hiyo pesa za kununulia wakulima mbolea. Pesa hizo sana hupitia Hazina Kuu ya Taifa.

Inapopelekwa katika kaunti hizo, wafadhili hao hutarajia kuwa serikali itafuatilia matumizi yake, ili zitekeleze malengo yaliyokusudiwa.

Suala nyeti limekuwa ni nani anayepaswa kutekeleza jukumu hilo la kufuatilia. Ndio sababu Bunge limebuni sheria iitwayo County Governments Grant Bill ya mwaka wa 2021.

Kifungu ya 96(3) cha Katiba yetu kinaeleza wazi kwamba jukumu la kusambaza pesa kwenye kaunti ni la Bunge la Seneti.

Mswada huo wa ugavi wa pesa za ruzuku ulianzishwa na bunge hilo, kama inavyotaka Katiba.

Inashangaza kwamba hata Hazina Kuu inakubaliana na Bunge la Kitaifa kuwa wabunge wawe na msemo katika ufuatiliaji wa pesa hizo.

Je, ina maana kuwa serikali sasa haiamini tena Katiba? Au wabunge wa seneti si watu wa kuaminiwa katika ufuatiliaji wa pesa zinazotumwa kwa kaunti? Kama maseneta waliopo sasa si waaminifu, Katiba hiyo hiyo inaeleza njia inayoweza kufuatwa ili kuwaondoa.

Haiwezekani kuwa wabunge, ambao kazi yao kubwa ni kuunda sera zinazoathiri shughuli za serikali ya kitaifa, watapewa kazi ya maseneta. Jambo linalozua wasiwasi ni kuwa, serikali haoni dosari yoyote katika suala hilo.

Mzozo kati ya seneti na Bunge la Kitaifa haujaanza jana. Kwa miaka sasa, kumekuwa na mvutano kuhusu mwenye mamlaka kumshinda mwenzake.

Katika kuzozana huko, mara nyingi ni wananchi katika kaunti ambao wameathiriwa. Pesa za kwenda kwa kaunti zimekuwa zikichelewa na kulazimu baadhi ya kaunti kukopa kwa riba ya juu.

Kama kweli serikali inaamini katika Ugatuzi, haina budi ila kuachia maseneta jukumu walilopewa na Katiba. Sheria yoyote inayohusu mambo ya kaunti, sharti iwahusishe kikamilifu maseneta.

Kufanya kinyume na hivyo ni kutaka kuifanyia Katiba mabadiliko kupitia mlango wa nyuma.

You can share this post!

Amerika yaionya Urusi dhidi ya kutumia silaha za kemikali...

GWIJI WA WIKI: Kennedy Wandera

T L