• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Amerika yaionya Urusi dhidi ya kutumia silaha za kemikali nchini Ukraine

Amerika yaionya Urusi dhidi ya kutumia silaha za kemikali nchini Ukraine

NA AFP

WASHINGTON, Amerika

RAIS wa Amerika Joe Biden amesema kuna dalili kwamba Urusi inapanga kutumia silaha za kemikali na kibayolojia nchini Ukraine, akionya kuwa mataifa ya Magharibi yataichukulia hatua ‘kali’ ikithubutu kutumia silaha hizo.

Akiongea jijini Washington Jumatatu jioni, Rais Biden alipuuzilia mbali madai ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba Amerika inahifadhi inaficha silaha za kemikali na kibayolojia katika mataifa washirika wake barani Uropa.

“Hii sio kweli, nawahakikishia,” aliuambia mkutano wa viongozi wa mashirika ya kibiashara jijini Washington.

“Pia wanadai kuwa Ukraine ina silaha ya kibayolojia na kikemikali nchini Ukraine. Hiyo ni ishara kwamba anapanga kutumia silaha aina hizi,” Rais Biden akaeleza.

Onyo kutoka Rais huyo wa Amerika lilifanana na taarifa iliyotolewa ka utawala wake mapema mwezi huu pamoja na mataifa mengine ya Magharibi.

Hii ni baada ya maafisa wa Urusi kuishutumu Ukraine kwa kuficha silaha za kemikali kwa usaidizi wa Amerika.

“Sasa ambapo Urusi imetoa madai haya ya uwongo… tunafaa kuwa chonjo kuhusu uwezekano wa kutumia silaha za kemikali au za kibayoloji katika vita vyao nchini Ukraine,” Msemaji wa Ikulu ya White House Jen Psaki akasema kupitia Twitter.

Jumatatu jioni, Rais Biden alisisitiza kuwa washirika wake wa Magharibi watachukua hatua “kali” dhidi ya Urusi ikidiriki kutumia silaha hizo zenye maadhara makubwa. Hata hivyo, hakufafanua hatua hizo.

“Putin anafahamu kutakuwa na matokeo hatari kwa sababu ya nguvu za pamoja za mataifa wanachama wa shirika la kujihami la NATO,” akasema bila kutaja hatua ambazo muungano huo utachukua.

Rais Biden aliongeza kuwa aliwahi kumwonya Putin kuhusu hatua ambazo Amerika itachukua ikiwa Urusi ifanya mashabulio ya kimtandao dhidi ya mitambo muhimu ya Amerika.

“Tulikuwa na mazungumzo kuhusu matokeo ya kitendo kama hicho,” akasema akirejelea mkutano kati yake na kiongozi huyo wa Urusi mwaka jana jijini Geneva, Uswizi.

Wakati huo huo, Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky jana Jumanne alisema yuko tayari kuwasilisha “masuala yote” ikiwa Rais Putin atakubali kufanya mazungumzo moja kwa moja naye kwa lengo la kukomesha vita hivyo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Zelensky alisema yuko tayari pia kuzungumzia suala la uthibiti wa maeneo yanayozozaniwa ya Crimea na Danbas.

Hata hivyo, Rais huyo alionya kuwa Ukraine haiku tayari “kusalimu amri” na kupitisha uhuru wake Urusi.

“Nikipata nafasi hii, na Urusi ikikubali, tutapitia maswali yote,” akasema kwenye taarifa iliyochapishwa katika shirika la habari la Suspilne.

“Je, tutaweza kuzisuluhisha zote? La. Lakini kuna nafasi kwamba… angalau tunaweza kusitisha vita,” Rais Zelensky akaongeza.

Kiongozi huyo alirejelea kauli yake ya awali kwamba Ukraine haitajiunga na NATO.

“Tumesitisha mipango yetu ya kujiunga na NATO lakini watu wetu hawatakubalia Kyiv idhibitiwe na Urusi. Hatutaachilia mji wa Kharkiv au mji wa Mariupol ulioathiriwa kwa mashambulio makali kutoka kwa wanajeshi wa Ukraine,” Zelensky akasema.

“Ukraine haitatimiza makataa ya Urusi,” akasisitiza

Jijini Kyiv, mapigano yaliendelea huku amri ya kutotoka nje kwa saa 35 ikitangazwa.

Hii ni baada ya wanajeshi wa Urusi kushambulia jumba moja la kibiashara na kuligeuza kuwa vifusi.

  • Tags

You can share this post!

N’Golo Kante ajiondoa katika timu ya taifa ya...

TAHARIRI: Serikali iwaachie maseneta kazi ya kufuatilia...

T L