• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
TAHARIRI: Serikali izidi kuweka hatua kuokoa waathiriwa wa baa la njaa

TAHARIRI: Serikali izidi kuweka hatua kuokoa waathiriwa wa baa la njaa

NA MHARIRI

HATUA ambazo serikali imechukua kukabiliana na njaa zinafaa kupongezwa.

Kiongozi wa nchi, Rais William Ruto, amekuwa msitari wa mbele kutoa kilio kwa washirika wa maendeleo kusaidia serikali kukabiliana na janga hili na kulingana na rais mwenyewe, waemeitikia wito kwa kupata serikali Sh20 bilioni.

Serikali ilikuwa imetenga Sh4.5 bilioni kwa shughuli hii na baada ya kushikwa mkono na washirika wa maendeleo, imeweza kupata pesa za kusaida Wakenya zaidi ya 4.5 milioni wanaokabiliwa na njaa.

Pesa hizi, pamoja na misaada mingine zikitumiwa vyema, zinaweza kupunguzia raia mateso yanayotokana na kiangazi cha muda mrefu. Miaka iliyopita, pesa za kusaidia raia masikini ikiwa ni pamoja na chakula cha msaada zilikuwa zikitumiwa visivyo na maafisa wa serikali waliopatiwa jukumu la kuzisimamia.

Maafisa kama hao hawafai kuvumiliwa kamwe. Kila mmoja anafaa kuunga hatua za serikali kuhakikisha raia walio kwenye hatari wanasaidiwa kwa kuwa hakuna anayejua kiangazi kinachoendelea kitaisha lini.

Serikali isilegeze kamwe juhudi za kusaidia waathiriwa wa ukame, wengi ambao wamepoteza kila kitu walichotegemea kujikimu kimaifa.

Huu ni wakati wa Wakenya kuungana kuokoa wenzao kutokana na hatari inayowakodolea macho kwa kuitikia wito wa serikali wa kuchanga walichonacho.

Ni makosa kwa raia wa sehemu kadha za nchi kuteseka huku walio na katika maeneo mengine katika nchi hiyo hiyo wakila na kubakisha.

Wakenya wamewahi kuungana kusaidia waathiriwa wa njaa na wanaweza kufanya hivyo tena mradi tu michango wanayotoa iwafikie wanaoihitaji.

Hata hivyo, serikali isiache mipango yake ya kutafuta suluhu ya kudumu kupitia miradi ya kujenga ustahimilivu kwa jamii za maeneo kame.

Kuna miradi mingi ambayo imekuwa ikitekelezwa na pengine wakati umefika kutathmimi ufaafu wake na kuondoa isiyo na faida na kubaini iwapo utekelezaji wake unafanywa ipaswavyo au inatumiwa kama mifereji ya kupatia watu wache utajiri.

Inatia moyo kusikia Rais Ruto akiahidi kuchimba mabwawa katika maeneo tofauti, mpango ambao unaweza kuhakikisha watu, mifugo na wanyama pori wana maji hata wakati wa kiangazi. Hivyo basi, haufai kusahauliwa baada ya mvua kunyesha na hali inayokumba nchi kwa sasa kubadilika.

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu bambam na mwanamitindo stadi

Wenye rekodi mbovu kwa CRB kulipa riba zaidi

T L