• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:46 PM
TAHARIRI: Sheria ya jinsia yafaa iangiliwe upya upesi

TAHARIRI: Sheria ya jinsia yafaa iangiliwe upya upesi

NA MHARIRI

JANA Jumatano mahakama iliipiga breki tume ya uchaguzi (IEBC) kuhusu agizo lake kuwa sharti vyama vya kisiasa vidumishe sheria ya thuluthi mbili (sheria inayohusu jinsia) katika uteuzi wa wawaniaji wa viti mbalimbali kwa uchaguzi mkuu ujao.

Hakika hilo haliwezekani kwa sasa hasa inapozingatiwa kuwa vyama vilishakamilisha mchujo majuma kadhaa yaliyopita, shughuli ambayo ni ngumu na ghali mno.

Zaidi ya hayo, wananchi ndio huwachagua wawaniaji wala sio vyama, hivyo basi kuvilazimisha kutekeleza agizo hilo ni hujuma.

Naam, Sheria ya Thuluthi Mbili iko katika katiba ya Kenya ya 2010 lakini ukweli ni kwamba uongozi wa taifa hili haujapata njia mwafaka ya kuitekeleza.

Ukweli ni kuwa hakika hakuna njia iliyo bayana ya kuitekeleza sheria hiyo.

Aidha, hatua ya katiba hiyo kubuni kiti cha Mwakilishi wa Kike katika kila kaunti ni ya kuhongerwa kwa sababu imesaidia pakubwa kutekeleza sheria hiyo, hata ingawa bado haijafaulu kwa asilimia mia moja.

Maadamu wananchi ndio huwateua viongozi watakaowania viti vya kisiasa katika vyama mbalimbali, itakuwa vigumu kuwalazimisha kuwateua watu wa jinsia fulani mahsusi.

Hii ni kwa sababu, wananchi huwateua wawaniaji kwa kutumia vigezo mbalimbali.

Miongoni mwa vigezo hivyo ni watu waliojitokeza kupigiwa kura ambao aghalabu huwa watu wa jinsia ya kiume kwa wingi, hasa nchini Kenya na kwingineko Afrika, kuliko wanawake.

Kwa hivyo, wananchi hawawezi kulazimishwa kuwachagua wanawake ambao hawajajitokeza kupigiwa kura.

Kigezo cha pili ni uwezo wao kuongoza. Hapa, kutokana na wingi wa wanaume wanaojitokeza kwenye mchujo na kisha uchaguzi, wengi wanaochaguliwa hatimaye huwa wanaume hao hao.

Vigezo vingine ni kama vile uwezo wa kuwashawishi wananchi na utajiri wa mali ambao kwa bahati mbaya wanaume huwazidia wanawake.

Hali hizo zinafanya iwe vigumu kutimiza sheria ya kijinsia. Je, nini kifanyike? Kwanza ili kutimiza amri hiyo, sharti sheria ibadilishwe ili kuunda viti zaidi vya uteuzi visivyohitaji uchaguzi ambavyo vitatengewa wanawake kimakusudi.

Pili, nafuu nyingine yaweza kuwa kubuni sheria mpya ya kuvihitaji vyama kutenga maeneo fulani kwa ajili ya watu wa jinsi isiyofikisha thuluthi moja.

You can share this post!

Ruto ajitetea katika kesi ya kushinikiza apokonywe wadhifa

Ruto, Raila bega kwa bega

T L