• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Ruto, Raila bega kwa bega

Ruto, Raila bega kwa bega

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto na mpinzani wake mkuu Raila Odinga wako nguvu sawa kwa umaarufu nchini.

Ripoti ya utafiti wa kura ya maoni uliofanywa na kampuni ya Nation Media Group wikendi iliyopita, inaonyesha kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga watapata asilimia 42 ya kura kila mmoja endapo uchaguzi utafanyika leo.

Matokeo ya utafiti ni ithibati kwamba kinyang’anyiro cha urais kitakuwa baina ya Dkt Ruto wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Bw Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya.

Utafiti huo ulioendeshwa na kampuni ya Infotrak Research & Consulting kati ya Mei 8 na 9, mwaka huu, unaonyesha kuwa ngome kuu za Naibu wa Rais ni Bonde la Ufa ambapo atapata asilimia 61 ya kura, Mlima Kenya (asilimia 60) na eneo la Ukambani (asilimia 40)

Ngome za Bw Odinga ni Pwani (asilimia 55), Kaskazini Mashariki (48), Magharibi (48), Nyanza (72) na Nairobi (51).

Asilimia 15 ya Wakenya ambao hawajaamua ndiyo itaamua atakayekuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta baada ya Agosti 9.

Ripoti hiyo, hata hivyo, inaonyesha kuwa wapigakura wanahitaji kiongozi mwenye tajriba na rekodi nzuri ya maendeleo bila kujali chama.

Asilimia 67 ya Wakenya wanaounga mkono Bw Odinga, walisema kuwa walivutiwa na tajriba yake katika masuala ya uongozi. Asilimia 53 ya wanaounga mkono Dkt Ruto pia walitoa sababu sawa na hiyo.

Asilimia 37 ya wanaounga mkono Dkt Ruto walisema kuwa walivutiwa na manifesto yake huku asilimia 29 wakisema kuwa walishawishiwa na manifesto ya Bw Odinga.

Wapigakura wanaovutiwa na miungano ya Azimio au Kenya Kwanza ni asilimia tano pekee.

Hiyo inamaanisha kuwa huenda miungano ya Kenya Kwanza na Azimio huenda ikapoteza viti vingi vya ugavana, useneta, ubunge na udiwani kwa sababu Wakenya hawatapiga kura kwa misingi ya vyama.

Vyama vidogo na wawaniaji wa kujitegemea huenda wakavuna viti vingi katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Ili kuibuka na ushindi, Dkt Ruto anafaa kupata angalau asilimia 90 ya kura katika eneo la Bonde la Ufa na Mlima Kenya.

Katika eneo la Bonde la Ufa, Dkt Ruto anafaa kukita kambi katika Kaunti za Nakuru, Kajiado, Narok, Turkana, Samburu ambapo Bw Odinga huwa akizoa kiasi kikubwa cha kura.

Ili Bw Odinga kuongezea kikapu chake cha kura atahitajika kupata angalau asilimia 90 ya kura katika eneo la Nyanza, haswa katika Kaunti za Kisii na Nyamira.

Bw Odinga pia anafaa kuhakikisha kuwa anavuna kiasi kikubwa cha kura katika ngome zake za Magharibi na Pwani.

Dkt Ruto pia atahitajika kupata zaidi ya asilimia 90 katika eneo la Mlima Kenya ambalo lilisaidia pakubwa Rais Kenyatta kupata ushindi katika chaguzi za 2013 na 2017.

Ikiwa Rais Kenyatta ataanza kupigia debe Bw Odinga Mlima Kenya, kuna uwezekano kwamba Dkt Ruto huenda akapata chini ya asilimia 70 ya kura za eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Sheria ya jinsia yafaa iangiliwe upya upesi

GWIJI WA WIKI: Martin Munene

T L