• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
TAHARIRI: Tuharakishe mipango ya kuangamiza viwavijeshi

TAHARIRI: Tuharakishe mipango ya kuangamiza viwavijeshi

NA MHARIRI

MWEZI huu wa Aprili kawaida huwa wakati ambapo mvua huanza kunyesha nchini.

Katika maeneo ya Pwani na Kati mwa nchi, mvua imeanza kushuhudiwa. Kunyesha huko kunaleta matumaini kwamba, huenda nchi ikajikwamua kutoka kwa kiangazi kinachoathiri maelfu ya wananchi.

Ukame unaendelea kushuhudiwa Kaskazini mwa Kenya, kukiwa na ripoti za vifo vya mifugo na binadamu kutokana na njaa na kiu.

Maeneo mengi ya Kaskazini hayajashuhudia mvua kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.

Ripoti zinaeleza kuwa wakazi wengi ambao utamaduni wao ni kuhamahama, sasa wametulia kwenye manyatta zao, wakivumilia makali ya njaa wakiwa hawana matumaini.

Kwa hivyo kuanza kunyesha kunaleta matumaini kuwa, huenda nchi ikapata chakula cha kutosha na kuwagawia wanaoathirika.

Lakini matumaini hayo yameanza kudidimia kutokana na ujio wa viwavi jeshi. Wadudu hao hatari wameripotiwa katika pembe zote za nchi. Maeneo ya Ukambani, wameanza kuvamia mimea michache inayochipuza.

Magharibi mwa nchi, wakulima waliopanda mahindi wanakaridia hasara. Wadudu hao wamevamia mahindi katika kaunti za Kakamega na Trans Nzoia, na kuzidisha uwezekano wa janga la njaa kusambaa nchi nzima.

Hofu hiyo inatokana na wadudu hao kuvamia mashamba ya mpunga eneo la Mwea, kaunti ya Kirinyaga.

Wadudu hao wameonekana katika kijiji cha Nderua ambako mchele hulimwa kwa wingi. Kulingana na wakulima wa mpunga, walianza kuona viwavi jeshi juzi tu ambao huenda waliingia katika mashamba yao kutoka kaunti jirani ya Murang’a.

Juhudi zao za kutumia dawa za kawaida za wadudu hazijafanikiwa. Viwavijeshi hao wanaendelea kuzaana kwa haraka na kuhatarisha kabisa uwezekano wa kupatikana mavuno.

Mradi wa ukuzaji mpunga wa Mwea hutoa asilimia 80 ya mchele unaotumiwa Kenya. Iwapo wadudu hao hawatakabiliwa haraka, huenda tukashuhudia hali ambapo tunaomba chakula cha msaada kutoka mataifa ya nje.

Tofauti na nzige ambao huvamia eneo moja na kuondoka, viwavi huendelea kula kila aina ya jani linalopatikana, na huendelea kuzaana na kuzagaa.

Wizara ya Kilimo yapaswa kuwaagiza maafisa wa vituo vya utafiti wa kilimo na wa wadudu, vitoe mwelekeo kuhusu mbinu bora za kuwaangamiza viwavi hao.

You can share this post!

Kilifi Ladies yaanza Ligi ya Kanda kwa kishindo

MWALIMU WA WIKI: Mdarisi mkwasi wa vipaji katika masomo ya...

T L