• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
MWALIMU WA WIKI: Mdarisi mkwasi wa vipaji katika masomo ya lugha

MWALIMU WA WIKI: Mdarisi mkwasi wa vipaji katika masomo ya lugha

NA CHRIS ADUNGO

SIRI ya kuchochea wanafunzi kuchangamkia masomo ni kuwasikiliza, kuelewa changamoto zinazowakibili na kuwaelekeza ipasavyo hatua kwa hatua.

Shughuli za ujifunzaji na ufundishaji zitakuwa rahisi iwapo mwalimu atatumia mbinu zitakazompa jukwaa la kushirikiana vyema na wanafunzi kutalii mazingira mbalimbali ya jamii inayowazunguka, kukuza viwango vya ubunifu na kuamsha ari ya kuthamini utangamano.

Zaidi ya majukumu ya kawaida ya kufundisha darasani, Bw Gichimu Njeri anashauri kuwa mwalimu ana wajibu mwingine wa kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi wake huku akiwatia shime wale wasiomudu somo lake kwa wepesi.

“Tambua uwezo wa kila mwanafunzi ndani na nje ya darasa. Wahimize wajitahidi zaidi katika hicho wanachokipenda kufanya,” anaeleza Gichimu.

“Mwalimu mkali hufanya wanafunzi wamwogope badala ya kumheshimu. Unapomfanya mwanafunzi kuwa rafiki wa karibu, atakuwa mwepesi wa kukufichulia panda-shuka zake. Nawe utapata fursa ya kubuni mbinu mwafaka za kumshajiisha na kumwelekeza vilivyo hadi afaulu katika kiwango chake binafsi,” anasema.

Gichimu alizaliwa mnamo Mei 7, 1991 katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru. Ndiye mwanambee katika familia ya Bi Susan Njeri.

Elimu

Safari yake ya elimu ilianzia katika shule ya msingi ya Moto, Molo (1998-1999) kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Mona, Molo (2000-2005). Alifanya KCSE kwa mara ya pili shuleni Molo mnamo 2010 baada ya kutofaulu vyema katika jaribio la kwanza 2009.

Ilikuwa hadi 2012 ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea shahada katika Isimu, Uanahabari na Mawasiliano (LMC). Alifuzu 2016 na akajiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) Bewa la Nakuru kusomea shahada ya ualimu baada ya kuhimizwa na waliokuwa walimu wake wa shule ya upili – Bw Okoth na Bw Wafula.

Mnamo 2009, Gichimu alitunga mashairi ya Kiingereza yaliyochapishwa katika kitabu ‘A World of Difference’ kwa udhamini wa shule ya Meadows, Uingereza.

Ilhamu ya kuchangamkia Kiswahili ilichangiwa zaidi na wanafunzi wenzake waliotambua umilisi na ukubwa wa uwezo wake katika Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa.

Malezi Bora

Dkt Robert Oduori wa Chuo Kikuu cha Moi ndiye alitangamana na Gichimu kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kumwamshia hamu ya kukichapukia Kiswahili baada ya kutambua utajiri wa kipaji chake katika utunzi wa mashairi ya Kiswahili na Kiingereza. Mwingine aliyemvuvia sanaa ya kutunga kazi bunilizi ni Bw Peter Njihia aliyemfundisha katika shule ya msingi ya Mona.

Gichimu alipata kibarua cha kufundisha katika shule ya Goshen Boys, Nakuru mnamo Septemba 2018. Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani yake katika umri mdogo. Alitunga mashairi ya Kiingereza mnamo 2009 na yakafana sana katika tamasha za kitaifa za muziki na drama. Mashairi machache ya Kiswahili, aliyoyatunga kwa ufundi mkubwa, yalimpandisha pia katika majukwaa mbalimbali ya tuzo za uandishi, akala na kushiba sifa kutokana na ubunifu wake.

Mnamo 2017, Gichimu aliandika miswada mitatu ya riwaya na kuwapokeza wachapishaji. Uliokuwa mswada wake wa tatu ulichapishwa na Storymoja Publishers kuwa riwaya ‘Pasha’ mnamo 2019. Mswada wa kwanza ulikataliwa na na ule wa pili ukazaa riwaya ‘Mkaidi’. Kazi zake nyingine ni novela ‘Kanda Shujaa wa Nyuni’, ‘Gharama ya Fanaka’ na ‘Baiskeli ya Kamaa’.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Tuharakishe mipango ya kuangamiza viwavijeshi

Mwaura hatimaye akubali matokeo ya mchujo Ruiru

T L