• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
TAHARIRI: Uhuru wa idara ya mahakama si suala la mzaha

TAHARIRI: Uhuru wa idara ya mahakama si suala la mzaha

NA MHARIRI

IDARA ya mahakama ni mojawapo ya nguzo tatu za serikali.

Nguzo nyingine ni bunge na urais unaojumuisha baraza la mawaziri.

Wataalamu huhimiza kuwa nguzo hizi tatu zishirikiane kwa kiwango fulani lakini muhimu zaidi kila mojawapo ipewe uhuru inaostahili ili kutenda kazi yake bila kuingiliwa.

Miongoni mwa nguzo hizo, uhuru wa mahakama huwa muhimu zaidi ya mihimili mingineyo.

Ili taifa listawi kiuchumi, mahakama ina wajibu mkubwa zaidi. Idara hii ndiyo hasa huwachukulia hatua wale wanaotenda uhalifu wa kiuchumi yaani ufisadi.

Iwapo haitaingiliwa, idara ya mahakama ina uwezo wa kuwapata na hatia waliopora mali ya nchi ni kuwapa adhabu, hasa kifungo, kulingana na uzito wa hatia yao.

Baadhi ya mataifa duniani kama vile Korea Kusini na China, imeripotiwa kuwa pindi inapobainika, kwa njia ya kisheria, kuwa mtu alihusika katika ufisadi, hatima yake si nyingine isipokuwa kumiminiwa risasi hadharani.

Huo ndio unaofaa kuwa mfano kwa mataifa yanayoendelea hasa barani Afrika. Mataifa mengi ya Afrika yamejulikana kwa viwango vya juu vya ufisadi ilhali hakuna adhabu yoyote ya dhati iliyotolewa dhidi ya wahalifu wanaohujumu ustawi wa nchi zao.

Hili huwa hivyo hasa kutokana na uhalisia kuwa wengi wanaoendeleza uhalifu huo, huwa ama viongozi wa kisiasa au wenye uhusiano wa karibu na viongozi wakuu serikalini.

Katika muktadha wa Kenya, rai imfikie Rais William Ruto kuwa wananchi wanategemea pakubwa juhudi zake katika vita dhidi ya ufisadi.

Kama njia ya kuikwamua Kenya kutoka kwenye lindi la kukopa madeni ya mara kwa mara hasa kwa mataifa ya kigeni, sharti mianya yote inayotumiwa kufyonza mali ya umma na watu wahatinafsi, izibwe.

Hilo linahitaji nia njema kutoka kwa viongozi wa serikali hasa wa ngazi ya juu.

Kwa kuziba mianya ya wizi wa mali ya umma, Dkt Ruto hatalazimika tena kuamuru idara za serikali zipunguze matumizi yake ya fedha ili zitumiwe kwa mahitaji mengine muhimu.

Pesa zitakuwapo za kutosha kulipa mishahara na kuendeleza miradi ya maendeleo kwa wakati mmoja.

Mantiki ya haya yote ni matukio ya hivi majuzi ambapo kesi nyingi kuhusu ufisadi zilizowasilishwa kortini wakati wa utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta, zimetupwa nje na washukiwa kuachiliwa huru.

Kuanguka kwa kesi nyingi kiasi hicho kunaweza kufasiriwa kama kuingiliwa kwa idara ya mahakama. Kama hali ni hiyo, basi ni bora ikomeshwe upesi.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge wa Thika apata maoni ya wakazi kuhusu NG-CDF

Malindi: Wanawake wafanya kazi za sulubu kwa bidii kukabili...

T L