• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Mbunge wa Thika apata maoni ya wakazi kuhusu NG-CDF

Mbunge wa Thika apata maoni ya wakazi kuhusu NG-CDF

NA LAWRENCE ONGARO

MKUTANO wa siku tatu wa wakazi wa Thika kujadili jinsi fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) zinavyostahili kutumika ulikamilika mnamo Ijumaa.

Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuangazia jinsi fedha hizo zilivyostahili kutumika mwaka wa 2022-23 na 2023-24.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a aliyehudhuria aliandamana na washikadau wengine kwa lengo la kupata maoni kamili ya wananchi kuhusu jinsi fedha hizo zinavyostahili kusambazwa.

Mbunge huyo aliwapongeza wale wote waliohudhuria vikao hivyo kwa sababu wananchi walipata fursa ya kujieleza ili shida yao iweze kutatuliwa kwa uwazi.

Alitoa hakikisho kuwa kila mzazi atakayejisajili kutaka fedha za NG-CDF kama basari atapata haki bila kubaguliwa.

“Wakati huu mimi kama mbunge wenu nitafanya juhudi kuona ya kwamba kila mzazi anampeleka mtoto wake shuleni hata ingawa fedha tunazopokea kutoka kwa Hazina Kuu ya serikali ni chache mno,” alisema mbunge huyo.

Alitaka serikali ifanye hima ili kutoa fedha za maendeleo za NG-CDF kwa sababu shule zitafunguliwa mnamo Januari 23.

Alisema eneo la Thika lina wapigakura wapatao 160,000 huku idadi ya watu kwa ujumla ikiwa ni 500,000.

“Kwa hivyo tunapata ya kwamba wazazi wanaotoka familia maskini hawapati fedha za kutosha ikilinganishwa na wale wenye uwezo wa kifedha,” alisema mbunge huyo.

Alisema eneobunge la Thika hupokea kiasi cha Sh130 milioni pekee ambapo ikilinganishwa na idadi ya wakazi wote wa Thika, fedha hizo ni chache mno.

Alisema kuna haja ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufanya juhudi kuona ya kwamba Thika inagawanywa hata mara tatu hivi ili wakati fedha za maendeleo zikitolewa, kuwe na uwazi na uwajibikaji wakati wa ugavi wa fedha.

Alipendekeza kuwe na shule mpya ya upili ya Jamhuri Secondary ili wanafunzi wengi kutoka Thika wapate nafasi ya kujiunga nayo bila kusafiri mbali.

Mwakilishi wa Wadi ya Hospital Bw John Njiru alipongeza mipango ya Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi ya kutaka kuigeuza Thika kuwa Super City.

Alipongeza kampuni ya Delmonte kwa kutoa ardhi ya ekari zaidi ya 560 ili kuipa sura mpya kaunti ya Kiambu.

Alisema viongozi wa Kiambu watazidi kumuunga gavana mkono ili afanikishe azma yake ya kugeuza mazingira yote ya Kiambu kwa mpangilio mwafaka.

“Jambo muhimu kwa wakati huu ni sisi kama viongozi tuje pamoja kwa kuzungumza kwa sauti moja ili mafanikio hayo yapatikane,” alifafanua Bw Njiru.

Alisema tayari gavana amezunguka kaunti yote ya Kiambu na kufanya mikutano na wananchi huku akielewa shida kadha zilizoko huko.

  • Tags

You can share this post!

Gavana wa zamani aagizwa ampe mwanamke Sh236,000 kila mwezi...

TAHARIRI: Uhuru wa idara ya mahakama si suala la mzaha

T L