• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
TAHARIRI: Wasichana walindwe dhidi ya ukeketaji

TAHARIRI: Wasichana walindwe dhidi ya ukeketaji

NA MHARIRI

LIPO kundi la siri eneo la Kati mwa Kenya ambalo ni tishio kuu kwa wanawake, hasa wasichana wadogo.

Hili ni dhehebu ambalo limetajwa kuwa lenye kuendeleza ukeketaji wa wasichana na wanawake na pia kuendeleza baadhi ya maovu ya kijamii.

Kwa zaidi ya miaka miwili, kundi hilo limekuwa likishinikiza kurejeshwa kwa baadhi ya desturi za kizamani za Gikuyu ambazo idadi kubwa ya watu, ambao ni vijana, hawazifahamu.

Wanachama pia wamekatishwa tamaa kutafuta matibabu hospitalini na kushauriwa kwenda kutafuta dawa za kienyeji.

Chanzo kikubwa cha wasiwasi kwa mamlaka husika za maeneo hayo ni siri na usiri unaozunguka shughuli za kikundi hicho.

Hakuna ubaya kukumbatia desturi za jadi, lakini kama zina matokeo mabaya ya kiafya au zimefichwa katika uhalifu, basi hazipaswi kamwe kuachwa ziendelee kuumiza wahusika.

Huu hasa ndio ubaya wa tendo hilo la ukeketaji.

Matambiko na shughuli za kitamaduni za zamani dhidi ya vijana wa kike wa jamii ya Agikuyu zimepigwa breki kutokana na madhara yake mabaya kwa wale wanaolazimishwa au kuvutiwa kukeketwa.

UNFPA imefafanua ukeketaji kama desturi ya kuondoa sehemu ya siri ya mwanamke kwa sehemu au yote kabisa, au kusababisha majeraha kwa viungo vya uzazi vya mwanamke, kwa sababu zisizo za kimatibabu.

Wataalamu wanaonya kwamba wasichana wanapokeketwa, wanakabiliana na hatari ya mara moja ya kuvuja damu, mshtuko, na majeraha makubwa wanapokabiliwa na maambukizi ambayo yanaweza kusababisha kifo kwa urahisi.

Kando na ukeketaji, kikundi kinajiingiza katika vitendo vingine vya vinadhalilisha na kunyanyasa wanawake.

Mamlaka lazima zichukue hatua haraka kuchunguza zaidi, kubaini walio nyuma ya kundi hilo, na kuchukua hatua madhubuti kulinda wanawake na wasichana.

You can share this post!

Sio wote wanafaa kusajili laini zao za simu- Chiloba

Rais apoteza washirika wake wakuu kwa Ruto

T L