• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Rais apoteza washirika wake wakuu kwa Ruto

Rais apoteza washirika wake wakuu kwa Ruto

NA CECIL ODONGO

RAIS Uhuru Kenyatta ameonekana kusalia mpweke katika eneo la Mlima Kenya baada ya waliokuwa washirika wake wakuu wa karibu kuhamia mrengo wa Naibu Rais William Ruto, uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ukikaribia.

Hatua ya Rais kumuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga inaonekana kuwasukuma wengi wa waliokuwa wandani wake katika chama tawala cha Jubilee kumhepa na kujiunga na United Democratic Alliance cha Dkt Ruto.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ndiye mshirika wa hivi punde zaidi kumtema Rais Kenyatta na kujiunga na Dkt Ruto.

Bw Muturi ambaye aliidhinishwa na chama cha Democratic Party kuwa mgombea urais wake, amekuwa karibu na Rais Kenyatta tangu 2002.

Bw Muturi alisema alijiunga na Kenya Kwanza baada ya kushauriana kwa upana.

“Nimesafiri maeneo mbalimbali ya nchi na ningependa kuthibitisha kuwa, Wakenya wengi wanapenda muungano huu ambao nimejiunga nao,” akasema Bw Muturi.

Alisema alikataa kuelekezwa mrengo wa kisiasa anaofaa kujiunga nao.

Wanasiasa wengine kutoka Mlima Kenya ambao walikuwa washirika wa Rais Kenyatta lakini wamemtema na kuingia UDA ni Gavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Muthomi Njuki (Tharaka-Nithi), Martin Wambora (Embu) na Mutahi Kahiga (Nyeri).

Maseneta Mwangi Githiomi (Laikipia), Irungu Kang’ata (Murang’a), Kimani Wamatangi (Kiambu) na Njeru Ndwiga (Embu) pia wapo kwenye mrengo wa Dkt Ruto.

Katika Kaunti ya Kiambu ambako ni nyumbani kwa Rais Kenyatta, ni wabunge watano pekee waaminifu kwa Jubilee huku wengine saba wakiegemea mrengo wa UDA.

Kwa ujumla, zaidi ya asimia 80 ya wabunge waliochaguliwa Mlima Kenya wamehama Jubilee na sasa wanampigia debe Dkt Ruto.

Akihutubia wakazi wa mtaa wa Pipeline eneobunge la Embakasi Kusini Jumapili iliyopita, Rais Kenyatta alionekana kutambua kuwa amehepwa na wandani wake na kuweka wazi kuwa hatabadilisha uamuzi wake wa kumuunga mkono Bw Odinga licha ya maasi yanayomkabili katika ngome yake.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Martin Andati, Rais alikosea kwa kumwachilia Dkt Ruto ajizolee umaarufu Mlima Kenya kupitia ziara nyingi alizofanya eneo hilo kati ya 2013 na 2017.

“Wakazi wengi wa Mlima Kenya wamevutiwa na siasa za Ruto kwa kuwa amekuwa karibu nao na kusikiliza kilio chao mara kwa mara. Tangu 2017 amezuru eneo hilo karibu mara 400 kwa michango ilhali Rais Kenyatta ametembelea eneo hilo mara chache sana kwa shughuli za maendeleo,” akasema Bw Andati.

Alisema eneo hilo linategemea kilimo na biashara, sekta ambazo zimeathirika pakubwa wakati wa utawala wa Rais Kenyatta ikilinganishwa na mtangulizi wake Mwai Kibaki.

Vilevile, Bw Andati alisema rais alimruhusu Dkt Ruto kudhibiti uteuzi wa Jubilee 2017 na kuzima ndoto za kisiasa za waliokuwa washirika wa rais ambao wangekuwa na usemi mkubwa katika siasa za urithi.

Hata hivyo, anahoji kuwa Rais akizidisha ziara zake mlimani na kufufua Jubilee, basi kuna uwezekano Bw Odinga atajizolea angalau asilimia 15 ya kura za Mlima Kenya.

“Kile ambacho kitamfaa Ruto dhidi ya Raila ni iwapo zaidi ya asilimia 90 za wakazi wa Mlima Kenya watajitokeza kupiga kura jinsi ilivyokuwa 2013 na 2017. Iwapo idadi itakuwa ndogo kisha ushawishi wa Rais umvunie Raila asilimia 15 za kura, Naibu Rais atakuwa taabani,” akaongeza Bw Andati.

Mtaalamu wa masuala ya sera na uongozi, Gabriel Muthuma naye anasema kuwa kilichomponza Rais Kenyatta ni kumakinikia masuala ya maendeleo tu bila kutoa mwelekeo kwa viongozi wa eneo hilo baada ya kura ya 2017.

“Ni kama Rais alifahamu hawanii kwa muhula mwingine ndiposa akashirikiana na Raila ili kufanikisha miradi ya serikali. Akitekeleza hilo, wanasiasa wa Mlimani walionekana kusalia yatima ndiposa wakaanza kujihusisha na Ruto na kuwarai wakazi wamuunge mkono,” akasema Bw Muthuma.

Anahoji kuwa, asilimia 80 za viongozi wa eneo hilo huwa hawachaguliwi tena jinsi ilivyokuwa 2013 na 2017 na kusema hata huenda mawimbi ya UDA yasiwafae wale ambao wamekuwa na utendakazi duni.

Hata hivyo, anakubaliana na Bw Andati kuwa idadi ya wapigakura watakaojitokeza kwenye uchaguzi wa Agosti 9 ndio itaamua mshindi kati Bw Odinga au Naibu Rais na kutoa hali halisi iwapo Rais Kenyatta bado anadhibiti Mlima Kenya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wasichana walindwe dhidi ya ukeketaji

MALEZI KIDIJITALI: Teknolojia yavutia wanaume kwa malezi

T L