• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
TALANTA: Dogo nguli wa Afrobeat

TALANTA: Dogo nguli wa Afrobeat

SHAUKU ya moyo wake ni kuwa mwanamitindo siku za majaliwa.

Amezamia kujituma kuchonga talanta yake kupitia kusakata densi na kuimarisha uelewa wake wa masomo ya lugha na jamii kuimarisha njia faafu za utangamano na uhusiano mwema kwani, anaamini hivyo ndivyo vigezo ambavyo vinaweza kumpatia upenyo.

Susan Wairimu,12, mwanafunzi wa darasa la nane mwakani shule ya msingi Junel, Kabete, Kaunti ya Kiambu anasema anapenda sana kusakata muziki wa Afrobeat kwani ndio unamchochea zaidi kupania kuwa mchezaji densi mahiri kwa sababu unamuongezea uwezo wa kujinengua kwa ustarabu sana. Hususan wimbo kama Girl Friends alioujengea msingi wa kusakata densi yake kwa sababu ni wimbo ambao unampelekea kutumia mitindo ya usakataji kusisimua wakati ambapo anausikiliza na kufuatilia biti zake kwa utaratibu huku akiibua mbinu za uchezaji densi.

Japo hubanwa na masomo, anasema wakati wa kujinoa huwa nadra.

Hata hivyo, hutumia wakati wake wa ziada kufanya mazoezi nyumbani na shule chini ya ushirikiano na wanagenzi wengine ambao husakata nao densi pamoja na kutumbuiza shuleni kukiwepo hafla au sherehe.

Aidha, yeye pia hushiriki katika ukariri wa mashairi kama njia mbadala ya kujikuza na kupata ukakamavu wa kusakata mbele ya hadhira.

Msakataji densi huyu anasema msakataji mzuri ni yule huwa mwenye kuangalia sana mifumo tofauti ya usakataji na kuona jinsi ambavyo anaweza kuikoleza katika mtindo wake. Mbali na ujuzi wake katika kufurahisha hadhira kwani ni kutokana na matumbuizo hayo msakataji hujichongea njia ya kupata ufuasi na ajira kwa sababu anaamini talanta inalipa ukiizingatia kwa mpana na marefu na kuweka bidii ya mchwa katika kujikuza zaidi.Isitoshe, yampasa mwanadensi kuwa yule anayeingia katika ulazima wa kukula chakula chenye lishe bora ili, apate nguvu, awe na uwezo wa kutafakari kwa haraka na kunywa maji mengi kuimarisha afya ya mwili wake.

Amepata sapoti kutoka kwa wazazi wake na wanafunzi wa darasa la nane kwani wamekuwa wakishirikiana nao kusakata densi shuleni. Fauka na kumtia moyo sana jambo ambalo lilimpa motisha zaidi ya kutambua umuhimu wa kuwa msakataji densi.

“Mzazi wangu hunikumbusha kuwajibika vyema ninapocheza densi.Hunihimiza kufanya kweli na kuhakikisha ninaendana na biti ya wimbo kupata mtiririko ulio mwema wa kucheza ndiposa uchezaji wangu uwe wa kusisimua,” anasema Wairimu.

Siku ambayo alifurahia ni wakati walikuwa na hafla ya kufuzu kwa wanachekechea shuleni ambapo walitumbuiza wazazi na wanafunzi kwa jazba sana.

Yeye hupenda kutizama kituo cha Kiss TV kujizolea mbinu za usakataji densi na jinsi ya kuwianisha mitindo.

Mnenguaji ambaye anamhusudu ni Kendi kutokana na vile anavyonogesha uchezaji wake.

Changamoto yake ni kusoma aina nyingine ya misakato ya densi kwani kuna nyingine ambazo huhitaji muda mwingi wa kumakinikia ndiposa uitoe miondoko ambayo inahitajika.

Kama hasomi wala kucheza densi, yeye hujifunza uanamitindo.

Ushauri wake ni kwamba, kama unataka kuwa mwanadensi na una uwezo kiasi, yakupasa kuwa makini na ujaribu kadri ya uwezo wako ukifuata sana maelekezo ya watangulizi wako na utapata njia muafaka ya kusakata densi.

You can share this post!

Ruto afuata nyayo za Moi katika kutawala

Cherera afeli kufika mwenyewe mbele ya JLAC

T L