• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Ruto afuata nyayo za Moi katika kutawala

Ruto afuata nyayo za Moi katika kutawala

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto amejitokeza kuwa mwanafunzi stadi wa mlezi wake wa kisiasa, Daniel Moi kwa kuiga mbinu alizotumia marehemu rais wa pili wa Kenya katika utawala wake wa miaka 24.

Rais Ruto alilelewa kisiasa na Mzee Moi akiwa mmoja wa viongozi wa kundi la vijana wa chama cha Kanu lililofahamika kama YK 92 (Youth for Kanu 1992).

Katika muda wa miezi miwili unusu ambayo amekuwa madarakani, Rais Ruto ametoa mwelekeo wake wa utawala ambao unatoa kumbukumbu za uongozi wa Moi.

Mkondo wa majuzi kabisa unaoashiria utawala wa Kenya Kwanza kumuiga Moi ni hatua ya kuwapatia machifu uwezo mkubwa mashinani.

Katika utawala wa chama cha Kanu, Moi aliwapatia maafisa wa utawala wa mikoa nguvu nyingi za kuhakikisha Wakenya walihisi nguvu za serikali.

Kila chifu alikuwa na maafisa wa polisi jinsi ambavyo serikali ya Kenya Kwanza imetangaza itafanya kwa kuwapa maafisa hao wa utawala mashinani maafisa watano wa polisi na silaha.

Mnamo Ijumaa, Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki alisema maafisa hao wa utawala watawezeshwa ili kutekeleza sheria na sera za serikali.

Hata hivyo, hofu imetanda kuwa huenda hatua hiyo ikarejesha Kenya katika enzi za Kanu, ambapo machifu walitumia nguvu zao kukadamiza haki za raia kwa kisingizio cha kutekeleza sheria na amri za serikali.

Kuwaongeza machifu nguvu ni kinyume cha Katiba ya sasa, ambayo imetwika polisi jukumu la kutekeleza sheria.

Kulingana na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Taifa, Opiyo Wandayi, serikali ya Kenya Kwanza inafanya maamuzi ya sera bila kufuata sheria kama alivyokuwa akifanya Moi.

“Tuko chini ya Katiba na sheria mpya. Katiba ya Kenya 2010 ilileta Sheria ya Huduma ya Polisi ikieleza wazi muundo wa polisi na hauhusishi machifu,” akasema Bw Wandayi.

Funzo lingine alilopata Rais Ruto kutoka kwa Moi ambalo anafuata kikamilifu ni kuchora picha ya kuwa Mkristo wa dhati kwa kuhudhuria ibada kila Jumapili na kupalilia uhusiano wa karibu na wahubiri.

Mara baada ya kuapishwa, Rais Ruto alialika wahubiri wa madhehebu mbalimbali Ikulu kufanya utakaso, ambapo Mama Taifa pia alitangaza maombi yatakuwa yakifanyika Ikulu kila mwezi.

Kila Jumapili Rais Ruto amekuwa akihudhuria ibada ambazo zinatangazwa kwenye mitandao na vyombo vingine vya habari moja kwa moja.

Mzee Moi katika utawala wake alikuwa pia akihudhuria ibada na habari hizo kutanguliza kwenye taarifa za KBC.

Katika utawala wake uliodumu kati ya 1978 na 2002, Mzee Moi alikuwa makini kufifisha upinzani kwa kushawishi wabunge wa vyama vingine kuvihama na kujiunga na Kanu. Punde baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Rais Ruto alianza juhudi za kufifisha upinzani kwa kushawishi baadhi ya wabunge wa upinzani na waliochaguliwa huru kujiunga na upande wa serikali.

Hatua yake ya kwanza ilikuwa ni kunyakua wabunge saba wa chama cha United Democratic Movement (UDM) katika juhudi za kuhakikisha upande wa serikali una wabunge wengi kuliko upinzani kuweza kupitisha miswada ya serikali.

Mnamo Ijumaa, vinara wa muungano wa Azimio One Kenya Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Martha Karua walishutumu Kenya Kwanza kwa juhudi za kurejesha utawala wa kiimla kwa kutumia Bunge.

Pia Rais Ruto anaonekana kutumia sera ya kigeni inayofanana na ya Moi kwa kukumbatia mataifa ya Ulaya na Amerika, tofauti na Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta ambao waliimarisha uhusiano na China. Hatua hiyo imezua malalamiko kutoka kwa Bw Odinga, ambaye amekuwa akilaumu serikali akiitaja kuwa mateka wa mataifa ya Ulaya na Amerika.

  • Tags

You can share this post!

Hasira polisi aliyehusishwa na ubakaji akitoweka

TALANTA: Dogo nguli wa Afrobeat

T L