• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
WANDERI KAMAU: Masharti mapya ya mchujo yasiwe jukwaa la ulipizaji kisasi

WANDERI KAMAU: Masharti mapya ya mchujo yasiwe jukwaa la ulipizaji kisasi

Na WANDERI KAMAU

UKOSEFU wa msingi thabiti wa kisiasa ni moja ya sababu ambazo zimeifanya Kenya kutokuwa na vyama vya kisiasa vyenye nguvu ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.

Hapa Kenya, ni vigumu kwa chama cha kisiasa kudumu kwa zaidi ya miaka 15.

Vile vinavyobahatika kukaa kwa muda huo, huwa vinahusishwa na mtu fulani mwenye ushawishi—ambaye kwa kawaida huwa “mmiliki” wa chama husika.

Ukosefu huo wa misingi bora huwa unadhihirika sana nyakati za shughuli za mchujo, ambapo wawaniaji huhama kutoka chama kimoja hadi kingine bila kuzingatia taratibu wala miongozo yoyote ya kisheria.

Hata hivyo, huenda hali hiyo ikabadilika mwaka huu baada ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu, kusema itakuwa vigumu kwa yeyote kuhama kutoka chama kimoja hadi kingine baada ya Machi 26.

Bi Nderitu alisema kuwa hiyo ndiyo itakayokuwa hatua ya kwanza katika “kulainisha na kusafisha” mazingira ya kisiasa nchini ambayo yamechafuka kwa muda mrefu.

Bila shaka, hii ni hatua nzuri, kwani itasaidia kuzima wanasiasa wenye mazoea ya kubadilisha vyama kama nguo nyakati za uchaguzi.

Ijapokuwa kumeibuka minong’ono katika baadhi ya kambi za kisiasa kuwa serikali inalenga kutumia kanuni hizo mpya kuwaadhibu wanasiasa ‘waasi’, wito mkuu wa Bi Nderitu ni kutokubali kutumika kama daraja la kuendeleza matakwa ya kisiasa ya baadhi ya mirengo.

Anapaswa kujitokeza wazi kudhihirisha afisi yake inaendesha majukumu yake bila mwingilio kutoka kwa idara yoyote ya serikali.

Hii itakuwa hatua muhimu ili kujenga imani ya raia kuhusu utendakazi wa afisi yake, hasa wakati huu uchaguzi unapokaribia.

Vivyo hivyo, kanuni hizo mpya zinapaswa kutekelezwa kikamilifu ili kuiwezesha Kenya kuboresha nidhamu yake ya kisiasa kama ilivyo katika nchi kama Tanzania na Afrika Kusini.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

NYOTA WA WIKI: Sadio Mane

Mwanafunzi aachiliwa kunyonyesha mtoto

T L