• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
NYOTA WA WIKI: Sadio Mane

NYOTA WA WIKI: Sadio Mane

NA GEOFFREY ANENE

SI ajabu kwamba Sadio Mane anasifika kama mmoja wa mawinga 10 bora duniani.

Ubunifu wake, ukatili mbele ya lango, visigino vya kutisha na kasi ya radi ni baadhi ya sifa zilizomfanya apate umaarufu tangu alipokuwa Red Bull Salzburg nchini Austria kati ya msimu 2012-2013 na 2014-2015.

Alianza uchezaji wa soka kijijini Bambali, Senegal, akiwa na umri wa miaka mitatu pekee.

Ndoto yake kubwa ilikuwa kusakata kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) aliyoitazama tu katika runinga.

Mane, ambaye alimpoteza baba mzazi akiwa mtoto mchanga, anatoka familia maskini.

Alihudhuria pia mechi za timu ya taifa lake kuona mashujaa aliowaenzi, na kuapa kuwa siku moja atakuwa kama wao.

Kilichomvutia zaidi kuzamia soka ni maajabu yaliyofanywa na Lions of Teranga kwenye Kombe la Dunia 2002.

Senegal ilifika robo-fainali ikishiriki dimba hilo kwa mara ya kwanza kabisa.

Winga wa Senegal Sadio Mane. PICHA | MAKTABA

Hiyo ni baada ya kuduwaza mabingwa wa dunia Ufaransa 1-0 na kulazimisha sare dhidi ya Denmark na Uruguay kwenye kundi lao, kabla kubandua Uswidi raundi ya 16-bora.

Mane alichukulia soka kwa uzito baada ya dimba hilo. Aling’ara kambini mwa akademia ya Generation Foot na kuwavutia maskauti wa soka kutoka Ufaransa.

Muda si muda alinyakuliwa na klabu ya Metz nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 15 mnamo 2011.

Alinawiri Metz kabla ya mchezo wake kwenye Olimpiki 2012 kusukuma Salzburg kumnyakua kwa donge la Sh518 milioni.

Misimu miwili baadaye, Southampton walimnunua kwa kitita cha Sh2.9 bilioni.

Zaidi ya mwaka mmoja na nusu baadaye, wakati huo akicheza katika kikosi kimoja na Mkenya Victor Wanyama, Mane alijiunga na miamba Liverpool kwa bei ya Sh5.3 bilioni.

Amefurahisha mno kambini Anfield baada ya kuchana nyavu mara 107 na kusuka pasi 44 zilizozalisha magoli katika mechi 244.

Kimataifa, Mane – ambaye majina yake ya utani ni Said na Ronaldinho – amechezea Senegal michuano 80; ameifungia mabao 29 na kuwa mfungaji bora kwa pamoja na mchezaji mstaafu Henri Camara.

Amewahi kujumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya mwanasoka bora duniani (Ballon d’Or).

You can share this post!

TAHARIRI: Wadau wakuu sasa fanyeni jambo Stars irejee...

WANDERI KAMAU: Masharti mapya ya mchujo yasiwe jukwaa la...

T L