• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
WANDERI KAMAU: Mdahalo wa urais uangazie sera zitakazoboresha maisha ya raia

WANDERI KAMAU: Mdahalo wa urais uangazie sera zitakazoboresha maisha ya raia

NA WANDERI KAMAU

MIDAHALO ya urais katika nchi zilizokomaa kidemokrasia kama Amerika kwa kawaida huangazia masuala ambayo wawaniaji watashughulikia ikiwa watafanikiwa kuchaguliwa kama rais.

Ingawa baadhi ya mataifa duniani yalipata uhuru baada ya Amerika, ni wazi kuwa Amerika imekuwa mfano bora katika kuendeleza demokrasia duniani, licha ya baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiiandama.

Midahalo hiyo huwapa raia fursa ya kuwatathmini kwa kina wagombeaji; sifa na sera zao. Ni majukwaa ambayo ni muhimu katika kuamua matokeo ya uchaguzi wa urais.

Yamkini Kenya imeanza kuiiga Amerika kwenye maandalizi ya uendeshaji wa midahalo hiyo.

Hata hivyo, kinyume na Amerika, ambapo wawaniaji huzingatia masuala na ajenda kuu za uchaguzi, hali inaonekana kuwa kinyume nchini.

Kwa mfano, kwenye Mdahalo wa Wawaniaji Wenza uliofanyika Jumanne katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki (CUEA), jijini Nairobi, wagombea wenza walionekana kujikita kwenye tofauti zao za kisiasa badala ya ahadi watakazowatimizia Wakenya ikiwa wataibuka washindi kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

Hilo lilijitokeza hasa kati ya Bi Martha Karua (mgombea mwenza wa Bw Raila Odinga katika muungano wa Azimio-One Kenya) na Bw Rigathi Gachagua, aliye mgombea-mwenza wa Naibu Rais William Ruto katika chama cha UDA.

Kwa mfano, badala ya Bw Gachagua kutumia muda wake mwingi kuelezea sera zao za kuboresha maisha ya Wakenya, aliutumia kuelezea anavyohangaishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wawili hao (Bw Gachagua na Bi Karua) walitumia karibu zaidi ya nusu ya muda waliotengewa kukosoana kwa misingi ya tofauti zao za kibinafsi na kisiasa.

Mwishoni mwa mdahalo huo, Bw Gachagua mwenyewe alikubali kuwa hawakuangazia masuala muhimu kama walivyotarajia.

Watu wengi walihisi Bw Gachagua alitumia nafasi hiyo kama jukwaa la kumwingilia Rais Kenyatta na familia yake, kama ambavyo amekuwa akifanya katika majukwaa mengine.

Bila shaka, wakati hisia kama hizo zinajitokeza, ni wazi midahalo hiyo inakosa kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Ikizingatiwa Wakenya wengi wanapitia hali ngumu kimaisha, suala kuu wanalotaka kusikia kwa sasa ni jinsi viongozi watafufua tena uchumi na kupunguza gharama ya maisha.

Ni wazi kuwa washindani wakuu kwenye uchaguzi huo wana tofauti kubwa za kisiasa.

Hata hivyo, hawapaswi kutumia jukwaa muhimu kama hilo kuleta tofauti hizo, kwani itakuwa ni sawa na kuwapotezea Wakenya wakati.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

USIU yalenga kumaliza mashindano ikiwa miongoni mwa timu...

CECIL ODONGO: Mizani ya kupima wawaniaji si upevu wa...

T L