• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2024 12:24 AM
WANDERI KAMAU: Mitandao imegeuzwa jukwaa la utapeli, wizi na upotoshaji

WANDERI KAMAU: Mitandao imegeuzwa jukwaa la utapeli, wizi na upotoshaji

Na WANDERI KAMAU

MOJA ya hatua ambazo dunia imepiga sana ni uwepo wa mtandao wa intaneti.

Kwa yeyote aliyeishi nyakati ambapo hakukuwepo na mtandao, maisha ya sasa huonekana kama muujiza wa aina fulani.

Kuna wakati mawasiliano yalikuwa kupitia barua pekee. Kuna nyakati mawasiliano ya simu yalikuwa ya watu matajiri pekee.

Kulikuwepo na nyakati ambapo redio ilikuwa kama thawabu vijijini—yaani, aliyeimiliki aliheshimika sana.

Nyakati hizo, runinga zilizokuwa vijijini zingehesabika.Mara nyingi, wale waliobahatika kuzimiliki walikuwa walimu au “watu walioajiriwa na serikali”, kulingana na simulizi zilizoendelea vijijini mwetu.

Hata hivyo, ugumu uliokuwepo kwenye mawanda ya mawasiliano uliondolewa na ujio wa mtandao wa intaneti na simu za rununu.

Kwa sasa, simu za rununu huwa kama afisi ndogo—mtu anaweza kufanyia chochote hapo.

Kwa mfano, anaweza kutuma au kupokea pesa, anaweza kusikiliza redio, kuweka jumbe mitandaoni, kufuatilia matukio mbalimbali duniani kama vile habari za kimataifa, kati ya masuala mengine.

Licha ya mazuri hayo yote yanayotokana na mitandao, ubaya ni kuwa baadhi ya watumizi wake wameigeuza kuwa jukwaa la wizi, ukandamizaji, upotoshaji na utapeli. Cha kushangaza ni kuwa, kinyume na wahalifu ambao hudukua mitambo ya benki na kupora fedha za wateja, ‘wezi’ wa mitandaoni wanatumia dini kuwapora raia.

Njama zao huwa mpango uliopangwa na kupangika.

Wale wanaohusika katika utapeli huo aghalabu huwa watu maarufu na wanaofahamika sana kwa watumizi wa mitandao, hasa ya kijamii kama Facebook.

Imebainika wao huzungumza na baadhi ya watu wanaopitia shida fulani, kwa mfano maradhi sugu kama saratani.

Wao huweka picha za watu hao kwenye kurasa zao, ambapo baadaye hutangaza kiasi fulani cha pesa kama gharama ya hospitali au karo ya masomo wanayohitaji ili kurudi shuleni.

Watu hao baadaye hutumia ushawishi kuwarai Wakenya au watumizi wa mitandao “kuwachangia” waathiriwa wa matatizo hayo.

Ingawa si michango yote ambayo imekuwa ikiendeshwa mitandaoni ni ya hila, baadhi imefichuliwa kuwa njama za watu wachache kujitajirisha.

Nimeibua suala hili baada ya mtu mmoja maarufu mitandaoni kudaiwa kupora pesa alizotumiwa kuwasaidia watoto mayatima.

Ingawa mtu huyo amejitokeza kujitetea kwa kila namna, tukio hilo linapaswa kuwafungua macho Wakenya kuwa, si kila mtu ajitokezaye kuwaomba usaidizi anapaswa kusikilizwa. Baadhi yao ni chui waliovalia ngozi za kondoo!

Kisa hicho pia kinapaswa kuwa changamoto kwa Bunge la Kitaifa kupitisha sheria itakayotoa mwongozo na kulainisha michango ya fedha inayoendeshwa mitandaoni.

Makala haya hayalengi kupiga vita michango hiyo, kwani kuna maelfu ya watu waliofaidika kupitia kwayo.

Wito mkuu kwa serikali, hasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), ni kuweka taratibu kali zitakazohakikisha kuwa yeyote anayejitokeza kuendesha michango kama hiyo ana kibali kutoka kwa idara husika.

Ikiwa hilo litatekelezwa, basi huo utakuwa mwanzo wa kuwaokoa Wakenya wenye huruma dhidi ya kulaghaiwa jasho lao na watu matapeli wasiowajali hata kidogo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wadau waepushe raia kususia kura katika uchaguzi...

KIKOLEZO: Ndoa za celebs bila jasho!

T L