• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
KIKOLEZO: Ndoa za celebs bila jasho!

KIKOLEZO: Ndoa za celebs bila jasho!

NA SINDA MATIKO

SAKATA ya juzi inayomhusu modo wa zamani Tanzania, Wema Sepetu kuchambwa na mbea wa Instagram Aristote kwamba dada kafulia kiasi kuwa hana usafiri wa binafsi, imeniibulia mjadala fulani.

Aristote aliamua kulinganisha maisha ya Wema na mwigizaji mwenzake Irene Uwoya. Hii ikiwa ni baada ya Irene kumwalika kwenda kula bata naye kwenye sherehe za bethidei yake na kutumia takriban Ksh1 milioni kujibamba na masela wake akiwemo mbea huyo.

Sasa katika kumsifia, Aristote alisema Wema hana uwezo wa kuishi kama Irene ambaye kando na kuwalisha bata la maana, anaendesha Range Rover wakati Wema akizunguka mji kwa teksi za Uber sababu hana gari.

Hili likanikumbusha jinsi maceleb wengi hupenda kufeki maisha hasa mitandaoni kwa kutaka kuaminishia watu kuwa maisha yao sio ya kawaida. Hii ni licha ya kuwa kwa ground vitu huwa tofauti kwani wengi wao huwa wanahangaika.

Ila kuna baadhi ya maceleb wanaoishi maisha yao ya uhalisia. Wengi wamedhihirisha haya kwa njia tofauti ikiwemo kuandaa harusi zao kwa bajeti ndogo mno.

ANGELINA JOLIE NA BRAD PITT

Bajeti: Dola 4,000 (Sh451, 000)

Mr and Mrs Smith walipoamua kuoana cha ukweli, harusi hiyo ilifanyika Agosti 2014. Kwa mastaa wa levo yao na utajiri walionao, kama wangelipenda, wangesafiri mpaka mwezini kutimiza shughuli hiyo.

Ila walichokifanya ni kuwaalika marafiki zao 22. Hawakuwafahamisha kwamba ilikuwa ni ndoa. Waliwaalika tu kuja kuhudhuria sherehe yao ndogo. Maua yaliyotumika hayakununuliwa ila yalichumwa kutoka kwenye bustani la boma lao. Gharama ya pekee waliyoingia ni ya manunuzi ya msosi ulioandaliwa na mpishi wao. Kwa bahati mbaya walitalikiana 2019.

BIEN BARAZA NA CHIKI KURUKA

Bajeti: Sh300,000

Baada ya zaidi ya miaka sita ya kudeti, Bien alimposa dansa Chiki na Machi 2020, wakaamua kuoana.

Ndoa ilifanyika chini ya maji kwenye afisi za Mkuu wa Sheria. Wakakabidhiwa cheti cha ndoa walichotia saini mbele ya mashahidi wao. Baada ya hapo, mke na mume wakaamua kuandaa karamu ndogo kwa ajili ya watu wao wa karibu. Ikatumwa mialiko ya kimya kimya.

Bien alimposa dansa Chiki na Machi 2020, wakaamua kuoana. PICHA | MAKTABA

Karamu ilifanyika katika bustani ya Pallet Cafe, mtaani Lavington, Nairobi. Walioalikwa hawakuzidi watu 200. Wote walioalikwa waliagizwa kuvalia nguo za Kiafrika na kufika sehemu fulani ambapo walipata wamesubiriwa na basi. Wote wakaagizwa kuacha simu zao na kisha kusafirishwa hadi eneo la tukio. Ndio sababu mpaka leo hamna picha za karamu hiyo zilizovuja.

Lakini kando na hayo, walitaka kuhakikisha kuwa kila mtu anafurahia pati bila ya usumbufu wa simu. Chakula kilikuwa cha kutosha na kwa wanywaji pombe kama wangependa, wangeoga nayo. Gharama kwa mujibu wa Bien, haikufika hata laki tatu.

EVERLYN WANJIRU NA AGUNDABWENI AKWEYU

Bajeti: Sh75,000

Kapo hii imedumu kwenye ndoa yao kwa miaka 10 sasa. Wanjiru ni staa wa muziki wa injili huku mume wake akiwa ni produsa na mwelekezi wa muziki.

Kwa muda huo, wameweza kuyaweka mahusiano yao siri kwani hata mitandaoni hutawakuta wakipostiana kila kukicha kama wenzao. Wanapenda zaidi kuzungumzia kazi zao zaidi ya maisha yao.

Hivi majuzi Wanjiru alifichua za ndani kuhusu ndoa yao akisema haikuwa ya gharama kubwa. Anasema walipoamua kufunga ndoa, hawakutaka kuingia gharama kubwa.

“Marafiki zetu walitusaidia tukachangisha Sh75, 000. Tukatumia Sh50, 000 kununua vyakula kisha Sh14, 000 kukodisha hema na viti. Kuna mpiga picha ambaye hakualikwa ila alikuja, ikawa basi tumwache ila atupe picha bila ya gharama yoyote. Pete tulinunua za kawaida tu zile za mtaani na zilitugharimu Sh500,” kanukuliwa.

Siku ya harusi walikuwa watumie gari moja la rafiki yao lakini jamaa akawatoka na kuwazimia simu. Hata hivyo walifanikiwa kupata lingine kutoka kwa mshirika wa kanisa. Shela alilovalia aliazima kutoka kwa mwanamke mmoja ambaye aliwahi kutumbuiza kwenye ndoa yake. Kapo hiyo haikuenda fungate baada ya harusi.

ESTHER KAZUNGU NA JAMES KIBUNJAH

Bajeti: Sh60,000

Vlogger na mcheshi wa mtandaoni Kazungu pamoja na mumewe Kibunjah walifunga pingu zao za maisha Septemba mwaka jana. Baada ya kudeti kwa miaka sita, waliamua wahalalishe kabisa mahusiano yao.

Walikwenda na kufunga ndoa yao mbele ya Mkuu wa Sheria ambayo kwa kawaida gharama huwa ni Sh3, 900 kwa mchakato wote.

Baada ya hapo waliandaa karamu ndogo ya marafiki zao na wanafamilia. Shughuli yote kwa ujumla ikawakosti Sh60, 000.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Mitandao imegeuzwa jukwaa la utapeli, wizi...

KASHESHE: Kimenuka Wasafi

T L