• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
WANDERI KAMAU: Njaa na umaskini ni maafa tuliyojiletea sisi wenyewe

WANDERI KAMAU: Njaa na umaskini ni maafa tuliyojiletea sisi wenyewe

MAISHANI mwangu, sijafanikiwa kwenda nchi za nje; ila katika enzi hii ya teknolojia, ni rahisi sana kufuatilia matukio yanayoendelea katika mataifa hayo.

Uwepo wa teknolojia na mtandao wa intaneti umewezesha kila mtu duniani kufuatilia matukio mbalimbali katika mataifa tofauti, wakati huu na miaka ya hapo awali.

Kwa mataifa yaliyostawi kiviwanda kama Amerika, Uingereza au Ujerumani, ni rahisi sana kufuatilia safari zake katika masuala ya kisiasa na kiuchumi kuanzia miaka ya zamani hadi katika kiwango yalichofikia.

Kwa Amerika, ufanisi wake haujakuwa rahisi. Imekuwa ni safari ndefu iliyokumbwa na changamoto nyingi sana. Kwa wakati mmoja, majimbo ya Kusini yalipigana na yale ya Kasikazini kati ya mwaka 1861 na 1865. Chanzo kikuu cha vita hivyo kilikuwa iwapo biashara ya utumwa ingepanuliwa hadi maeneo zaidi au la.

Hata hivyo, mzozo huo uliisha 1865 baada ya Rais Abraham Lincoln kushinda uchaguzi wa urais. Alianza mchakato wa kuyaunganisha majimbo hayo kwa kutatua masuala tata.

Nchini Uingereza, hali ni iyo hiyo. Ni falme ambayo ina historia ndefu ya karne kadhaa. Hivyo, safari yake kufikia ufanisi ilio nao kwa sasa imechukua zaidi ya miaka 100.

Nchini Ujerumani, simulizi ni kama hizo. Kabla ya Ujerumani Mashariki na Magharibi kuungana kuwa taifa moja mnamo 1989, kulikuwa na uhasama mkali baina ya pande hizo mbili.Yote tisa, linalojitokeza ni kuwa mataifa haya ya ng’ambo hayajafikia ufanisi wake virahisi.

Hapa Kenya, inasikitisha kuwa baada ya karibu miaka 60 ya kujinyakulia uhuru, bado tunakumbwa na changamoto zile zile tulizokuwa nazo 1963.

Alipoongoza harakati za uhuru, hayati Mzee Jomo Kenyatta alisema lengo lake kuu lilikuwa kukabili njaa, umaskini na ujinga.

Miaka 60 baadaye, Kenya imekwama pale pale ilipokuwa 1963: Njaa, umaskini na ujinga!Picha za baa la njaa linalokeketa Kaunti ya Turkana na maeneo mengine nchini, ni ishara ya nchi isiyojali kabisa mustakabali wake!

Turkana ni miongoni mwa kaunti ambaz-o zimekuwa zikipokea fedha nyingi zaidi kutoka kwa Serikali Kuu tangu mfumo wa ugatuzi uanze kutekelezwa nchini mnamo 2013.

Huwa haipokei chini ya Sh10 bilioni kila mwaka, kwa kuzingatia takwimu za fedha zinazotolewa kwa kaunti.

Ni vipi tena watu wanakufa kutokana na makali ya njaa? Ni hali ya kutojali? Mbona tusijifunze na mataifa kama Amerika, Uingereza ama Ujerumani?

Hii ni aibu tuliyojiletea sisi wenyewe. Ni mwiba wa kujidunga ambao kamwe hauambiwi pole.

  • Tags

You can share this post!

Wanaofichua wachafuzi mazingira Nairobi kutuzwa

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tunamshukuru Allah kwa kututeremshia...

T L