• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tunamshukuru Allah kwa kututeremshia mvua

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tunamshukuru Allah kwa kututeremshia mvua

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam, maswahaba wake na watangu wema hadi siku ya Qiyaama.

Ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu, tupo katika kipindi kigumu mno. Lipo baa la njaa ambalo limezua mahangaiko! Ukame kila kona! Njaa. Vifo. Dhiki na matatizo chekwachekwa!

Wiki jana kuliandaliwa swala maalum, ambapo waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu, tulinyenyekea na kumlilia Mola. Na sasa baadhi ya maeneo nchini yamejaaliwa mvua. Alhamdulillahi. Ni nini zaidi tunahitaji kujua wazi kuwa Mola anatupenda, na Uislamu ndio dini ya haki?

Je, swala hii huandaliwa vipi?

Tunanukuu: Swala ya kuomba mvua ni rakaa mbili, bila ya kuadhini wala kukimu, na kisomo katika rakaa mbili hizo huwa ni kwa sauti. Mwenye kuswali katika rakaa ya kwanza atapiga takbiri saba baada ya ile takbiri ya kufungia swala. Na katika rakaa ya pili atapiga takbiri tano, mbali ya ile takbiri ya kuinuka kutoka kwenye sijida.

Mwenye kuswali atainua mikono yake katika kila takibiri, atamhimidi Mwenyezi Mungu na kumsifu na atamswalia Mtume (SAW) baina hizo takbiri. Baada ya kuswali imamu atahutubu hutuba moja, atakithirisha kuomba msamaha na kusoma Kurani katika hiyo hutuba. Kisha ataomba kwa wingi dua zilizopokewa, pamoja na kukariri na kurudia maombi na kuonyesha unyonge, uhitaji na umasikini kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka, na ainuwe mikono yake upeo wa kuinua.

Imamu ataelekea Kibla na ataendelea kuomba baina yake yeye na Mola wake.Kila ugonjwa una tiba yake, ardhi ikiwa kavu na kupatikana ukame. Uislamu umeweka ibaada Maluum nayo ni (Swalatul IstisQai) ni Swala ya kumuomba Mwenyezi Mungu kuteremsha mvua.

Leo Swala hii imesahulika kabisa katika Umma wa kislamu. Waislamu wakipata matatizo ya uhaba wa Mvua, moja kwa moja wanaelekea kuomba majini na mashetani. Mafundisho ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam yako wazi kabisa kuwaelekeza Waislamu katika njia ya Allah (Subhaanahu wa Taala) wakati wowote na hali yoyote sawa wakati wa raha au shida.

Kitendo hiki cha kufanya maombi maalum ya kuwepo kwa mvua ni sunnah iliyotiliwa mkazo kwa kitendo cha Mtume (SAW) kama ilivyo kwenye hadithi iliyopokelewa na Abdullah bin Zaid kwamba Mtume (SAW) alitoka kwenda kwenye kiwanja cha kuswali akaomba mvua, akaelekea Kibla, na akaswali rakaa mbili). Imepokelewa na Bukhari na Muslim.

Zikinyesha mvua, inatakiwa kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu ijaalie (iwe) yenye kumiminika yenye kunufaisha.”

Je, mimi na wewe, matajiri na mabilonea, tunatumia vipi utajiri wetu kuonesha hisani kwa wahanga wa njaa na ukame?

Au tunazidi kufanya israfu kwa kumwaya ovyo maji, vyakula, kula na kuvimbiwa hadi kushindwa kupumua, ilhali wenzetu wanakonda, kudhoofishwa na kuuliwa kwa njaa?

Je, unapokuwa nyumbani na unatizama kwenye runinga makala ya jinsi waja walivyoathirika kutokana na ukame, huwa unapigwa na mshipa wa utu? Au habari za baa la njaa kwenye redio kwako wewe na mimi ni kama tu maji ya mkondo yakijiendea?

Ya Rabi tuepushe na janga hili la ukame, kama ambavyo wewe hutuepushia mbali mjanga aina aina.Ijumaa Kareem!

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Njaa na umaskini ni maafa tuliyojiletea sisi...

Naibu Chansela wa KU arejea chuoni kwa kishindo

T L