• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:55 AM
WANDERI KAMAU: Tutathmini upya mchakato mzima wa kuomboleza marais wanaofariki

WANDERI KAMAU: Tutathmini upya mchakato mzima wa kuomboleza marais wanaofariki

NA WANDERI KAMAU

WAKATI mwingine, taratibu zinazozingatiwa na jamii katika masuala tofauti huwa zinazua maswali mengi ikiwa zinafaa ama hazifai.

Katika hali hiyo, jamii hujikuta kwenye njiapanda—kuhusu namna taratibu hizo zitaathiri vizazi vijavyo ama zitawaathiri wanajamii wenyewe.

Ni hali ambayo pia inaibua mjadala kuhusu jamii inafaa kuzifutilia mbali baadhi ya taratibu za kigeni zinazokinzana na mienendo yake.Suala hili limeibuliwa na baadhi ya makundi ya watu, yanayokosoa mtindo wa kuwaweka marais wanaofariki kwenye mabunge ili kutazamwa na raia.

Kwa vizazi vilivyopo nchini (vilivyozaliwa baada ya 1978), mtindo huu ulikuwa jambo jipya kwao 2020, baada ya marehemu Daniel Moi kuwekwa bungeni kwa siku tatu, ili kuwaruhusu Wakenya kuutazama mwili wake na kumpa heshima zao za mwisho.

Kwa wale walioona tukio hilo kwa mara ya kwanza, ulikuwa mshangao mkubwa.

Wengi walihisi kama jambo lisilofaa, kwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa tamaduni za Kiafrika kuweka maiti mahali wazi ili kutazamwa na watu.

Jambo hili limejirudia tena—kwani mwili wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki uliwekwa bungeni kati ya Jumatatu na Jumatano kuwaruhusu Wakenya kuutazama.

Kama ilivyokuwa wakati wa kifo cha Bw Moi, maswali yale yale yameibuliwa: Je, mtindo huu unafaa? Hata ingawa ni hali ya kawaida katika nchi wanachama za Jumuiya ya Madola, nafasi yake i wapi miongoni mwa jamii na tamaduni za Kiafrika?

Bila shaka, hili ni swali lenye uzito kwa kuwa hatuwezi kamwe kuutenga Uafrika tunapoendesha taratibu zinazotokana na mitindo ya kigeni kuwaaga wapendwa wetu.

Kuligana na taratibu zilizopo, rais yeyote (aliye mamlakani ama aliyestaafu) huwa hana usemi kuhusu jinsi atakavyozikwa, kwani mara tu baada ya kifo chake, huwa anageuka “mali” ya jeshi na nchi husika.

Familia huwa haina usemi wala ushawishi mkubwa kuhusu taratibu zitakazozingatiwa.

Hata hivyo, pengine umewadia wakati utaratibu huu utathminiwe upya, kwani asili yake ni nchini Uingereza.

Baadhi ya maswali yanayoibuliwa ni: Ikizingatiwa Mzee Kibaki alikuwa mtu mwenye usiri mkubwa katika maisha yake, yalikuwa matamanio yake kuzikwa kwa utaratibu huo?

Mbona asizikwe kwa usiri huo, hata ikiwa alihudumu kama rais?

Katika maisha, pengine ni uumbaji wake Mungu pekee—kwa mfano jua linavyochomoza na linavyotua—ambao mwanadamu hana uwezo wa kuubadilisha.

Hata hivyo, kuna nafasi kubadili na kutathmini upya taratibu zinazotumiwa kuyaendesha masuala yanayoihusu jamii.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Serikali iwekeze zaidi katika miradi ya...

KIPWANI: Toto la Kitaita lateka anga ya uigizaji

T L