• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:15 AM
WANDERI KAMAU: Uhuru hafai kutumia lugha ya mama katika vikao vya umma

WANDERI KAMAU: Uhuru hafai kutumia lugha ya mama katika vikao vya umma

NA WANDERI KAMAU

KWA kipindi cha miaka 15 aliyochowala Kenya, kati ya 1963 na 1978, Mzee Jomo Kenyatta hakuwahi kutumia lugha asili ya Gikuyu kuwahutubia raia katika majukwaa ya umma.

Badala yake, Mzee Kenyatta alikuwa akitumia Kiswahili au Kiingereza kuwahutubia wananchi, viongozi ama wajumbe kutoka ng’ambo waliomtembelea Ikulu ya Nairobi.

Wanahistoria wanasema Mzee Kenyatta alitumia lugha yake asili tu alipokutana na washirika wake wa karibu— wengi wakiwa wanasiasa maarufu waliomzunguka kutoka Kaunti ya Kiambu.

Hali ilikuwa hiyo kwa marehemu Daniel Moi.

Kwa miaka 24 aliyoiongoza Kenya kati ya 1978 na 2002, ni mara chache mno ambapo Mzee Moi alinukuliwa akiwahutubia wenyeji wa Bonde la Ufa kwa lugha ya Kikalenjin.

Mzee Moi alikuwa Mtugen. Daima, alihutubu kwa Kiswahili au Kiingereza.

Hata wakati wa kampeni, Mzee Moi alikuwa akitumia Kiswahili, akiwarai Wakenya kukikumbatia kama lugha ya taifa.

Rais Mstaafu Mwai Kibaki aliwaiga watangulizi wake, na alipenda kutumia Kiswahili au Kiingereza kila wakati.

Bw Kibaki hakuwahi kutumia lugha ya mama hadharani. Hata hivyo, hali ni kinyume kwa Rais Uhuru Kenyatta, ambapo tofauti na watangulizi wake, amekuwa akitumia lugha ya Gikuyu kila anapowalenga wenyeji wa Mlima Kenya.

Ingawa Rais Kenyatta ni mwanasiasa, baadhi ya wananchi wanahisi amekuwa akitumia vibaya majukwaa ya umma kwa kuwahutubia wenyeji kwa lugha asili bila kujali hadhira inayomtazama.

Kwa mfano, alipowahutubia wenyeji wa eneo hilo Jumanne iliyopita katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Rais Kenyatta alitazamwa na maelfu ya Wakenya. Ingawa aliomba radhi, akieleza sababu ya kutumia lugha hiyo, Rais Kenyatta alikosa kuonyesha ufaafu wake kama kiongozi wa kitaifa.

Ingawa matumizi ya lugha asili miongoni mwa wanasiasa ni jambo la kawaida katika nchi tofauti duniani, matumizi hayo hulingana na historia, uthabiti wa kisiasa na mustakabali wa nchi ama jamii husika.

Nchini Tanzania, raia wanaunganishwa na lugha ya Kiswahili, hivyo si vigumu kwa kiongozi yeyote kuamua lugha atakayowahutubia raia nayo.

Katika nchi za Ulaya kama Ujerumani, Uingereza, Ureno, Uhispania kati ya nyingine, viongozi wa mataifa hayo hutumia lugha asili kuwahutubia raia, kwa kuwa hayana historia za jamii kugeukiana kwa misingi ya tofauti zao za kikabila.

Mataifa hayo pia yamekuza lugha zao katika kiwango cha kimataifa. Hata hivyo, hali ni tofauti Afrika, ambapo raia huwa wanapigana kwa misingi ya kikabila.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Msajili wa Vyama akaangwa kwa kuzembea kusafisha orodha ya...

CHARLES WASONGA: Kalonzo alisaliti Mudavadi,...

T L