• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
WANDERI KAMAU: Wakati ni sasa kwa kina mama kujikweza na kutwaa uongozi

WANDERI KAMAU: Wakati ni sasa kwa kina mama kujikweza na kutwaa uongozi

NA WANDERI KAMAU

TANGU 1992, baada ya Kenya kukumbatia mfumo wa siasa za vyama vingi, idadi ya wanawake ambao wamekuwa wakijitosa kwenye ulingo wa siasa imekuwa ndogo mno.

Kama jamii nyingine za Kiafrika, wanawake wamekuwa wakichukulia siasa kama jukwaa au “kazi” ya wanaume pekee.

Ndiposa licha ya mabadiliko mengi ya sheria ambayo yamekuwa yakifanywa nchini tangu mwaka huo ili kuongeza idadi ya wanawake kwenye siasa, si mafanikio mengi yaliyofikiwa kufikia sasa.

Kwenye uchaguzi wa 1992, ni wanawake wachache tu, kama vile kiongozi wa Narc-Kenya Bi Martha Karua, walifanikiwa kuchaguliwa kama wabunge.

Hali hiyo ilijirudia kwenye uchaguzi wa 1997.

Hata hivyo, hali iliimarika mnamo 2002, baada ya idadi ya wanawake waliochaguliwa kama wabunge, hasa katika eneo la Bonde la Ufa, kuongezeka pakubwa. Mafanikio yao yaliongezeka, baada ya hayati Mwai Kibaki kuteua wanawake kadhaa kama mawaziri na manaibu wao.

Ilikuwa nadra kwa tawala za hapo awali kuona mwanamke akishikilia wadhifa wenye ushawishi mkubwa serikalini kwa mfano, kama waziri.

Baadhi ya wanawake walioteuliwa na Rais Kibaki kuhudumu kama mawaziri ni Bi Karua, Gavana Charity Ngilu (Kitui) na Bi Linah Jebii Kilimo.

Upeo wa mafanikio ya wanawake kwenye ulingo wa siasa nchini ulikuwa ni kupitishwa kwa Katiba ya sasa ya 2010.

Katiba hiyo iliweka msingi thabiti kuhusu nafasi ambazo wanawake, vijana na walemavu wanapaswa kutengewa katika taasisi zote za umma na kibinafsi.

Ni baada ya utekelezaji wa Katiba hiyo ambapo Kenya ilianza safari mpya ya kutambua umuhimu na mchango wa wanawake katika nyanja za kisiasa, kijamii, kitamaduni, kimasomo kati ya nyingine. Kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, wanawake watatu walifanikiwa kuchaguliwa kama magavana. Wao ni Bi Ngilu (Kitui), Bi Anne Waiguru na marehemu Joyce Laboso (Bomet).

Mwaka huu, idadi ya wanawake waliojitokeza kuwania nafasi muhimu kama ugavana, ubunge na udiwani imeongezeka maradufu.

Kando na ugavana, wawaniaji watatu wa urais kati ya wanne wameteua wanawake kama wagombea-wenza wao. Bila shaka, hili linatufunza kuwa, wanawake wameanza kupata usemi nchini kama ilivyo kwingineko duniani.

Ingawa kwa kiwango kikubwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na mageuzi ya kikatiba, huu ndio wakati mwafaka kwa wanawake kutumia nafasi hiyo kupanua zaidi ushiriki wao kwenye siasa na masuala mengine muhimu ya ustawi wa nchi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ije na mikakati mipya kubabili utumizi...

TALANTA: Dogo mtelezaji

T L