• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
TALANTA: Dogo mtelezaji

TALANTA: Dogo mtelezaji

NA RICHARD MAOSI

NCHINI Kenya bado kuna uhaba wa wachezaji katika spoti ya kuteleza kwa viatu vya magurudumu almaarufu kama skating, huu ukiwa ni mchezo wenye asili ya ughaibuni hususan katika majira ya baridi.

Hata hivyo, kuna baadhi ya makinda chipukizi ambao wanaibukia, mojawapo akiwa ni Myra Faisal mwenye umri wa miaka minne, wa shule ya msingi ya Children of Freedom inayopatikana eneo la Lanet kaunti ya Nakuru.

Faisal ambaye vilevile huchezea timu ya Sprint Skating Club Kenya kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 10 anasema kuwa amejiwekea malengo ya kuwa mchezaji wa kimataifa siku za usoni.

Ingawa Faisal hajakuwa mzoefu sana, anasema amekuwa akijifundisha kwa kufanya mazoezi katika barabara laini ya shule na kila siku ya Jumapili yeye hujumuika na wachezaji wenzake katika ukumbi wa Standard Chartered Grounds Nakuru mjini.

Kulingana na Faisal, huu ni mchezo ambao unampasa mshiriki kudumisha hali ya juu ya nidhamu na kutunza saa wala asisahau kufanya mazoezi ili kujinoa vilivyo.

“Mchezo wa magurudumu ya kuteleza hunisaidia kuwa mkakamavu na kunipa nguvu,”asema, akiongeza kuwa kuna manufaa mengineyo kama vie kusaidia mtu kuwa mmakinifu hata zaidi.

Aidha anasema kuwa kupitia kwa mchezo huu, amefanikiwa kujitambua na vilevile kuletea shule yake tuzo nyingi, ikiwa ni pamoja na kuongezea jina lake hadhi.

Miongoni mwa michezo ya hadhi ya juu ambayo amewahi kushiriki ni Two Rivers Skate iliyofanyika jijini Mombasa, na mchuano wa Skating for The Course uliofanyika Kasarani kaunti ya Nairobi mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa Faisal, mara ya kwanza haikuwa rahisi kujitosa katika mchezo huu kwani unahitaji nguvu nyingi , bidii na mazoezi ya kutosha.

Katika hatua ya kwanza mchezaji atahitaji mandhari mazuri ya kuteleza, kisha hatua kwa hatua, ashirikishe ubunifu ili kukwepa mategu na matuta yanayopatikana njiani.

Pili, anasema kuwa ni muhimu kuzingatia usalama wakati wa kushiriki mchezo wa skating, ambapo wazazi wake wamemnunulia head gear, viatu vya magurudumu na sare rasmi.

“Vilevile, ili kudumisha usalama wa kiwango cha juu, kinga madhubuti zinahitajika katika sehemu za magoti na viwiko vya mikononi,”alisema.

Anamalizia kwa kusema mchezo wa viatu vya magurudumu ya kuteleza ni njia ya kipekee ya kutuliza ubongo baada ya wiki nzima shuleni badala tu ya kushinda akitazama runinga kila wikendi.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Wakati ni sasa kwa kina mama kujikweza na...

PAUKWA: Bahati aonea soni kovu usoni pa mama

T L