• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
WANTO WARUI: Tabia ya wabunge inafurisha vichwa wanafunzi wanaoshiriki utovu wa nidhamu

WANTO WARUI: Tabia ya wabunge inafurisha vichwa wanafunzi wanaoshiriki utovu wa nidhamu

NA WANTO WARUI

TABIA iliyoonekana hivi majuzi bungeni ya kuzua fujo na kupigana katika bunge la kitaifa ni jambo la aibu kabisa na kielelezo kibaya kwa watoto wetu hasa wanafunzi ambao wameanza kuvimba vichwa na kuonyesha visa vingi vya utovu wa nidhamu.

Huku tukiendelea kutafuta shuluhisho la kudumu la kudhibiti utovu wa nidhamu shuleni, wabunge wetu ambao tunawaita waheshimiwa ndio walio katika mstari wa mbele kuzua fujo na kuvunja sheria kwa kupigana. Ikiwa ‘Waheshimiwa’ wanashindwa kuafikiana katika mazungumzo yao na kuzua fujo, ni vipi tunatarajia wanafunzi wawe watulivu?

Baadhi ya wanafunzi nchini ni watoto wa wabunge hawa na wanapowaona wazazi wao wakionyesha ubabe wao kwa kupigana, bila shaka watafanya vivyo hivyo shuleni. Inasemwa kuwa mwana hufuata kisogo cha nina.

Wakati ambapo jamii imekosa kuwa kielelezo bora kwa watoto wake, hasa wale watu ambao ni viongozi, basi ni dhahiri kuwa matendo maovu yanayofanywa na watu hao yanaashiria jinsi nchi itakavyokuwa siku za baadaye. Hapana shaka kuwa wabunge wawa hawa wanaopigana bungeni ndio waliopitisha sheria bungeni kupinga wanafunzi kuchapwa viboko shuleni. Aidha wamekuwa katika mstari wa mbele katika kupitisha sheria dhidi ya dhuluma za kinyumbani. Basi hiki ni kinaya cha aina gani hao wenyewe kupigana bungeni?

Katiba ya Kenya inasemekana kuwa mojawapo ya zile nzuri barani Afrika. Ikiwa katiba hii inaruhusu matendo kama haya kutendeka hasa bungeni, basi bara letu lingali katika siku za giza na haliko karibu kuuona mwangaza. Wabunge kama hawa wanaopigana bungeni wanafaa kufikishwa mahakamani mara moja, wahukumiwe na wapoteze viti vyao vya ubunge maana hawafai tena kuitwa waheshimiwa.

Udhaifu wa sheria aidha huonyesha udhaifu wa watu waliounda sheria hizo. Je, wabunge tunaowachagua wamefikia viwango? Elimu humfanya mtu kuwa mstaarabu na mwenye maadili. Je, wabunge wetu wana elimu ya kutosha inayoafikiana na mahitaji ya kuongoza jamii? Ikiwa hakuna vigezo mwafaka vilivyowekwa vya kudhibiti wanasiasa na matendo yao, basi raia wengine watafuata tabia walizo nazo hao watunga sheria.

Ikiwa tuna haja ya kudhibiti nidhamu katika shule zetu, basi ni sharti viongozi wawe katika mstari wa mbele kudumisha amani.

na kuwa kielelzo bora kwa wanafunzi. Viongozi wanaoonyesha vitendo hasi hawawezi kamwe kujenga jamii yenye maadili. Maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana kamwe ikiwa jamii haina mshikamano, umoja na amani.

Kenya ni nchi ambayo imekuwa na misingi bora ya amani na tusingependa kuwafunza watoto wetu njia mbovu za vita na fujo ili kutatua matatizo. Nchi nyingi zimeangamia kwa ajili ya jambo hili.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Amerika, Ulaya zijue shida za kiusalama ziko...

Penalti ya Sadio Mane yasaidia Senegal kuzamisha Zimbabwe...

T L