• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Penalti ya Sadio Mane yasaidia Senegal kuzamisha Zimbabwe katika mechi ya Kundi B kwenye AFCON

Penalti ya Sadio Mane yasaidia Senegal kuzamisha Zimbabwe katika mechi ya Kundi B kwenye AFCON

Na MASHIRIKA

PENALTI ya sekunde za mwisho wa kipindi cha pili kutoka kwa fowadi Sadio Mane wa Liverpool iliwezesha Senegal kukomoa Zimbabwe 1-0 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi B kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON).

Kichapo hicho kilikuwa kichungu zaidi kwa Zimbabwe waliowabana vilivyo wapinzani wao ambao ni miongoni mwa vikosi vinavyopigiwa upatu wa kutawazwa mabingwa wa AFCON mwaka huu.

Penalti hiyo ambayo Senegal walipokezwa ilitokana na tukio la Kelvin Madzongwe kunawa mpira alioelekezewa na Pape Gueye ndani ya kijisanduku.

Senegal ambao wanaorodheshwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) katika nafasi ya kwanza barani Afrika, walitandaza mchuano huo bila beki Kalidou Koulibaly wa Napoli na kipa Edouard Mendy wa Chelsea. Wawili hao ni miongoni mwa wachezaji wanane wa Senegal wanaougua Covid-19.

Mbali na Mane, kiungo Gana Gueye anayechezea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa, pia alipoteza nafasi nyingi za wazi katika kipindi cha kwanza licha ya kusalia uso kwa macho na kipa Petros Mhari wa Zimbabwe.

Senegal ambao ni wanafainali wa AFCON 2002 na 2019, wanawania ufalme wa kipute hicho kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, uthabiti wao umetikiswa na visa vya maambukizi ya corona na majeraha kiasi cha kusalia na wanasoka 17 pekee kati ya 28 waliotajwa na kocha Aliou Cisse katika kikosi chake cha awali.

Ingawa hivyo, walishuka dimbani kwa matao ya juu huku kiungo mvamizi wa Bayern Munich, Bouna Sarr na fowadi Keita Balde wakishuhudia makombora yao katika kipindi cha kwanza yakigonga mwamba wa lango la Zimbabwe.

Ushindi wa Senegal ulinyima Zimbabwe fursa ya kukamilisha mechi ya AFCON kwa mara ya kwanza bila kufungwa bao katika jaribio la 13 kwenye kipute hicho.

Senegal wanaowania taji la kwanza la AFCON katika jaribio lao la 16 wamedumishwa na FIFA katika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa wiki 38 mfululizo. Sasa wako pazuri zaidi kusonga mbele kwa hatua ya 16-bora kutoka Kundi B linalojumuisha pia Malawi na Guinea.

Guinea wanaoshikilia nafasi ya 81 kimataifa, walikuwa wanafainali wa AFCON 1976. Uwepo wa Naby Keita (Liverpool), Amadou Diawara (Roma), Ilaix Moriba (RB Leipzig) na Aguibou Camara (Olympiakos) kikosini mwao kunatarajiwa kuwavusha kirahisi hadi raundi ya 16-bora pamoja na Senegal.

Zimbabwe (121) wananogesha fainali za AFCON kwa mara ya tano mara hii huku wakilenga kupiga hatua zaidi baada ya kudenguliwa kwenye makundi mnamo 2004, 2006, 2017 na 2019. Malawi (129) watafungua kampeni zao dhidi ya Guinea baadaye usiku wa leo. Watakuwa wakijaribu bahati ya kusonga mbele zaidi ya hatua ya makundi kwa mara ya tatu baada ya kubanduliwa mapema mnamo 1984 na 2010.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa benchi ya kiufundi kambini mwa Malawi, Mario Marinica, kikosi hicho kitategemea zaidi idadi kubwa ya masogora wanaocheza katika ligi yao ya nyumbani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WANTO WARUI: Tabia ya wabunge inafurisha vichwa wanafunzi...

Wakulima wahimizwa kukumbatia mifumo bora kudhibiti athari...

T L