• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
WANTO WARUI: Ufunzaji kupitia mtandao usiwe njama ya kutoajiri walimu kama inavyohofiwa

WANTO WARUI: Ufunzaji kupitia mtandao usiwe njama ya kutoajiri walimu kama inavyohofiwa

NA WANTO WARUI

JUMA lililopita, Tume ya kuajiri walimu nchini (TSC) kupitia kwa Afisa Mkuu Mtendaji wake Bi Nancy Macharia ilitoa tangazo kwamba kutakuwa na mafunzo ya wanafunzi wa sekondari kupitia mtandaoni ili kuziba pengo la ukosefu wa walimu katika shule za sekondari.

Bi Macharia alisema kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa wanafunzi wa sekondari walio katika shule ambazo hazina walimu wa kutosha.

Akielezea jinsi ambavyo shughuli hiyo itatekelezwa, Bi Macharia alielezea kuwa mafunzo yataendelezwa kiteknolojia kwa njia ya mtandao kutoka katika Shule ya Wavulana ya Alliance na ile ya Wavulana ya Machakos.

Walimu wa shule hizo mbili watakuwa wakipeperusha masomo wanayofunza shuleni mwao hadi shule husika.

Licha ya kuwa tunaishi katika wakati wa utandawazi na hatuwezi kuepukana na matumizi ya mtandao siku hizi, kuna hatari ya jambo kama hili hasa pale linapojaribiwa kwa wanafunzi.

Tatizo lililopo la uhaba wa walimu shuleni haliwezi kutatuliwa kupitia kwa njia ya mtandao pekee.

Kuna maelezo ambayo humhitaji mwalimu kuwasiliana na wanafunzi wake moja kwa moja ili yaeleweke ipasavyo.

Ingawa hii ni hatua nzuri ya maendeleo katika sekta hii ya elimu, uangalifu unafaa kuzingatiwa sana tusije tukavuruga elimu.

Maelezo ya Bi Macharia kuwa, licha ya masomo hayo ya mtandaoni TSC itaendelea kuajiri walimu yanazua hofu kwa walimu.

Suala la ukosefu wa walimu wa kutosha si geni katika nchi hii. Serikali haijaweza mpaka sasa kuajiri walimu wa kutosha wa kushughulikia idadi kubwa ya wanafunzi katika shule zetu.

Hivyo basi, hii isiwe ni njama ya kutowaajiri walimu zaidi au kupunguza waliomo kwani serikali imekuwa ikisukumwa ipunguze mishahara ya wafanyakazi wake na mashirika kama vile Benki ya Dunia.

Upungufu wa walimu shuleni haujasababishwa na ukosefu wa walimu kwani hata sasa kuna walimu wengi sana nchini ambao hawajaajiriwa.

Vyuo vya walimu na vyuo vikuu vinaendelea kutoa mafunzo kwa walimu huku idadi ya walimu inayoajiriwa kila mwaka ikiwa ndogo sana.

Hata kama mafunzo haya ya mtandaoni yatatekelezwa ipasavyo, pengo linalostahili kuzibwa halitawezekana kwani elimu itakayotolewa haitakuwa imekamilika.

Kuna masomo kama vile Kemia, Kilimo na mengineyo ambayo yanahitaji ufunzaji wa mwanafunzi akiwa papo kwa hapo na mwalimu wake.

Kivyovyote vile, TSC inapeleka elimu katika kiwango kingine kwa kupiga hatua ya masomo mtandaoni kwa kutumia teknolojia.

Hata hivyo, hii isiwe ni njama ya kupunguza walimu shuleni au kisingizio cha kutowaajiri wengine.

  • Tags

You can share this post!

Mwanaharakati aliyezima BBI sasa kugombea useneta Migori

Everton wateua Frank Lampard kuwa kocha wao mpya

T L