• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:27 AM
Everton wateua Frank Lampard kuwa kocha wao mpya

Everton wateua Frank Lampard kuwa kocha wao mpya

Na MASHIRIKA

KOCHA wa zamani wa Chelsea, Frank Lampard, atahudumu ugani Goodison Park kwa miaka miwili na nusu ijayo baada ya kukubali kurithi mikoba ambayo Everton ilipokonya mkufunzi Rafael Benitez mnamo Januari 16 kutokana na matokeo duni.

Lampard sasa anasuka benchi mpya ya kiufundi itakayomsaidia kunyanyua Everton waliosajili ushindi mara moja pekee kutokana na mechi 13 chini ya Benitez aliyejiunga nao mwanzoni mwa msimu huu.

Lampard, 43, alipiku wakufunzi Mreno Vitor Pereira na Duncan Ferguson kwenye mahojiano yaliyoandaliwa na Everton mnamo Ijumaa iliyopita.

Sajili wa kwanza wa Everton chini ya kocha Lampard ni kiungo raia wa Uholanzi, Donny van de Beek aliyetokea Manchester United kwa mkopo mnamo Jumapili.

Wasaidizi wa Lampard kambini mwa Everton watakuwa Joe Edwards anayetokea Chelsea pamoja na Paul Clement aliyewahi kufanya kazi na mkufunzi Carlo Ancelotti katika klabu za Everton, Chelsea, Paris Saint-Germain (PSG), Real Madrid na Bayern Munich.

Lampard ambaye pia amewahi kunoa kikosi cha Derby County, alipigwa kalamu na Chelsea mwanzoni mwa mwaka 2021 baada ya kuhudumu ugani Stamford Bridge kwa miezi 18. Kazi ya Everton ni ya kwanza kwa mkufunzi huyo raia wa Uingereza tangu wakati huo.

Kibarua chake cha kwanza kambini mwa Everton ni kibarua kitakachowakutanisha na Brentford katika raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Januari 5, 2022 uwanjani Goodison Park. Everton watavaana na Newcastle United ugani St James’ Park katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wiki moja baadaye.

Katika kipindi chake cha misimu 13 ya usogora kambini mwa Chelsea, Lampard aliwajibishwa mara 648 na akazolea miamba hao mataji 11 yakiwemo manne ya EPL na moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012.

Katika msimu wake wa kwanza wa ukufunzi ugani Stamford Bridge, aliongoza Chelsea kuambulia nafasi ya nne ligini na kutinga fainali ya Kombe la FA. Hata hivyo, vichapo vitano kutokana na mechi nane katika msimu uliofuata vilichangia kutimuliwa kwake.

Wayne Rooney wa Derby County, Sean Dyche wa Burnley, Paulo Fonseca aliyewahi kumezewa mate na Tottenham Hotspur na Newcastle United, Kasper Hjulmand wa timu ya taifa ya Denmark na Jose Mourinho wa AS Roma ni wakufunzi wengine waliohusishwa pakubwa na mikoba ya Everton baada ya Benitez kupigwa kalamu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WANTO WARUI: Ufunzaji kupitia mtandao usiwe njama ya...

Nyota Shikangwa na Awuor watambulishwa rasmi Uturuki,...

T L