• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
AC Milan wachabanga Benevento na kudhibiti tena kilele cha jedwali la Serie A

AC Milan wachabanga Benevento na kudhibiti tena kilele cha jedwali la Serie A

Na MASHIRIKA

AC Milan waliwadengua Inter Milan kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kuwapiga Benevento 2-0 licha ya kusalia uwanjani wakiwa na wachezaji 10 baada ya Sandro Tonali kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 33.

Franck Kessie aliwaweka AC Milan kifua mbele kupitia penalti ya dakika 15 kabla ya Tonali kufurushwa uwanjani kwa kosa la kumchezea Artur Ionita visivyo. Ingawa awali Kessie alikuwa ameonyeshwa kadi ya manjano, maamuzi hayo yalibatilishwa na adhabu kali zaidi kutolewa baada ya refa kurejelea tukio hilo kupitia video ya teknolojia ya VAR.

Rafael Leao aliwafungia Milan bao la pili katika 49 na kuwasaidia waajiri wake ambao wamejizolea alama 37 kutokana na mechi 15 kufungua mwanya wa alama moja kati yao na Inter Milan kileleni mwa jedwali.

Gianluca Caprari wa Benevento alipoteza mkwaju wa penalti iliyopanguliwa na kipa Gianluigi Donnarumma. Penalti hiyo ilitokana na hatua ya Caprari kukabiliwa visivyo na Rade Krunic ndani ya kijisanduku.

Chini ya kocha Filippo Inzaghi, AC Milan walivurumisha makombora 25 langoni mwa Benevento japo mashambulizi hayo hayakuzalisha bao lolote katika kipindi cha pili.

AC Milan ambao kwa sasa hawajapoteza mechi kati ya 15 zilizopita wameratibiwa kupepetana na Juventus mnamo Januari 6 uwanjani San Siro.

  • Tags

You can share this post!

Pigo kwa waandalizi wa Michezo ya Shule baada ya Rais Uhuru...

BBI: Matakwa ya Waislamu kwa Raila