• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
AC Milan wachapa Verona na kuwakaribia Inter Milan kileleni mwa jedwali la Serie A

AC Milan wachapa Verona na kuwakaribia Inter Milan kileleni mwa jedwali la Serie A

Na MASHIRIKA

AC Milan waliwapokeza Hellas Verona kichapo cha 2-0 mnamo Machi 7, 2021 na kuwajongea Inter Milan wanaonolewa na kocha Antonio Conte kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Licha ya kukosa huduma za mvamizi mzoefu Zlatan Ibrahimovic anayeuguza jeraha, Milan walijituma vilivyo na kutia kapuni alama tatu zilizowadumisha katika nafasi ya pili kwa alama 53, tatu pekee nyuma ya Inter.

Ingawa hivyo, nafuu zaidi kwa Inter ni kwamba wana mechi moja zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya michuano ambayo imesakatwa na Milan wanaotiwa makali na mkufunzi Stefano Pioli.

Milan walifungua ukurasa wa mabao kupitia frikiki ya Rade Krunic katika dakika ya 27 kabla ya Diogo Dalot anayewachezea kwa mkopo kutoka Manchester United kuongeza la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Matokeo hayo yaliwawezesha Milan kufungua pengo la alama nne kati yao na mabingwa watetezi Juventus ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 52, mbili mbele ya AS Roma wanaofunga orodha ya nne-bora.

Chini ya Conte, Inter huenda wakafungua tena mwanya wa pointi sita kileleni mwa jedwali la Serie A mnamo Machi 8, 2021 iwapo watashinda mechi yao ya nyumbani dhidi ya Atalanta ambao kwa sasa wanakamata nafasi ya tano kwa alama 49.

Milan waliowaendea Verona wakijivunia kusajili ushindi mara moja pekee kutokana na mechi nne za awali ligini, walikuwa kileleni mwa jedwali kuanzia Oktoba 2020 hadi Februari 2021 na kwa sasa wanafukuzia taji lao kwa kwanza baada ya ukame wa miaka 10 taji la Serie A.

MATOKEO YA SERIE A (Machi 7, 2021):

Verona 0-2 AC Milan

Roma 1-0 Genoa

Crotone 4-2 Torino

Fiorentina 3-3 Parma

Sampdoria 2-2 Cagliari

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wamiliki wa hoteli na baa Machakos waiomba serikali iondoe...

Newcastle United waridhishwa na sare tasa dhidi ya West...