• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Newcastle United waridhishwa na sare tasa dhidi ya West Brom ligini

Newcastle United waridhishwa na sare tasa dhidi ya West Brom ligini

Na MASHIRIKA

KOCHA Steve Bruce wa Newcastle United alikuwa mwingi wa sifa kwa masogora wake baada ya kuwalazimishia West Bromwich Albion sare tasa katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililowakutanisha mnamo Jumapili ugani The Hawthorns.

Licha ya Bruce kukosa huduma za wanasoka wake watatu tegemeo katika mechi hiyo, Newcastle waliondoka uwanjani na alama moja iliyowawezesha kuwaruka Brighton na kupaa hadi nafasi ya 16 kwa alama 27.

Sasa ni pengo la alama moja ndilo linawatenganisha Newcastle na Brighton ambao wamejizolea idadi sawa ya alama na Fulham waliowapepeta Liverpool 1-0 katika mechi nyingine ya Jumamosi ligini.

Callum Wilson, Miguel Almiron na Allan Saint-Maximin ambao wamehusika moja kwa moja katika mabao 16 ambayo yamefungwa na Newcastle katika mechi 27 zilizopita ligini, walikosa kuwa sehemu kilichotegemewa na Bruce dhidi ya West Brom.

Kukosekana kwao kulifanya Bruce kutegemea pakubwa maarifa ya Ryan Fraser, Joelinton Lira na Joe Willock.

“Niliridhishwa na ukomavu wa kikosi na kiwango cha kujituma kwa kila mchezaji. Wanasoka walionyesha kiu ya kutaka kusajili ushindi na kupata alama muhimu ili kuepuka presha ya kuingia ndani ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho. Matokeo hayo yalikuwa ya kuridhisha ikizingatiwa wingi wa visa vya majeraha kambini mwetu kwa sasa,” akasema Bruce.

Newcastle ndio waliopata nafasi nyingi zaidi za kufunga mabao katika mechi hiyo iliyomshuhudia kipa Sam Johnstone akifanya kazi ya ziada kupangua makombora mazito ya Jonjo Shelvey na Willock.

Sare hiyo iliwasaza West Brom katika nafasi ya 19 kwa alama 18, nne pekee mbele ya Sheffield United walio katika hatari ya kushushwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Bruce alimleta uwanjani fowadi Dwight Gayle katika kipindi cha pili na ujio wake ukazidisha kasi ya mchezo katika safu ya mbele. Gayle alifungia West Brom jumla ya mabao 23 katika Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) misimu miwili iliyopita.

Mechi dhidi ya Newcastle ilikuwa ya tatu kwa West Brom kukamilisha bila ya kufungwa bao. Kikosi hicho kwa sasa kimejivunia alama sita kutokana na mechi tano zilizopita, moja kuliko idadi ya alama walizojizolea katika mechi 10 za kwanza chini ya ukufunzi wa kocha Sam Allardyce.

West Brom kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote ya ligi kati ya tatu zilizopita dhidi ya Newcastle kwa mara ya kwanza tangu Januari 2005.

Newcastle kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Aston Villa katika mechi ya EPL mnamo Machi 12 ugani St James’ Park huku West Brom wakiwaendea Crystal Palace mnamo Machi 13, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AC Milan wachapa Verona na kuwakaribia Inter Milan kileleni...

Wananyuki yazidi kuwika baada ya kuwanyuka wapinzani wao wa...