• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
AFROBASKET: Kenya Morans yalenga kumaliza ukame wa miaka 28

AFROBASKET: Kenya Morans yalenga kumaliza ukame wa miaka 28

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Morans imeapa kufanya kila iwezalo kumaliza ukame wa miaka 28 nje ya Kombe la Bara Afrika la mpira wa vikapu la wanaume (AfroBasket) itakaposhiriki mechi za kufuzu mnamo Februari 19-21.

Mechi hizo za Kundi B, ambalo linajumuisha Kenya, Senegal, Angola na Msumbiji, zitaandaliwa jijini Yaounde, Cameroon.

Morans itakuwa bila kocha Cliff Owuor, ambaye aliajiriwa na klabu ya APR nchini Rwanda, ingawa imepata kocha Liz Mills kutoka Australia.

Katika mahojiano na Shirikisho la Mpira wa Vikapu Afrika (FIBA), Valentine Nyakinda alikuwa na imani tele kuwa uzoefu ambao timu hiyo ilipata katika mechi za mkondo wa kwanza nchini Rwanda mwezi Novemba 2020, utakuwa muhimu katika kampeni za Morans kumaliza ukame huo.

Nyakinda alieleza kuwa kile Morans inafaa kufanya ni kuchukulia kila mchuano kwa uzito unaofaa na kupigana hadi kipenga cha mwisho.

Nyota huyo wa klabu ya Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA) anaamini kuwa Kenya itatuma onyo kali kwa wapinzani wengine barani Afrika katika kampeni yake ya Cameroon.

Nyakinda alichangia pakubwa katika raundi ya kwanza akitumiwa mara nyingi kama mchezaji wa akiba. Uweledi wake ni katika kufunga mpira kutoka nje ya mduara pamoja na kurejesha nyavuni mipira ambayo haijaingia.

Alieleza kuwa Morans ilijifunza kutokana na makosa mengi iliyofanya na itaonyesha mchezo tofauti mjini Yaounde.

“Mjini Kigali, ilikuwa mara yetu ya kwanza kucheza dhidi ya majina makubwa kama hayo, lakini wapinzani ni wale wale kwa hivyo hatutatikisika. Tumegundua kuwa ni mpira ule wa vikapu tunaofahamu,” alieleza shirikisho hilo baada ya kipindi kimoja cha mazoezi.

Nyakinda aliongeza kuwa Kenya kurejea kwenye dimba la AfroBasket kwa mara ya kwanza tangu 1993 ni ndoto iliyo hai.

Mshambuliaji huyo mwenye urefu wa mita 2.01, ambaye amekuwa katika timu ya taifa tangu 2014, anasema makubwa yako njiani.

“Nafasi zetu za kuingia AfroBasket ni nzuri sana. Tunajitahidi kutimiza lengo hilo. Tunachostahili kufanya ni kufanya mazoezi makali na kuweka akilini mwetu kuwa inawezekana.”

Kenya ilihangaisha Senegal katika robo tatu za kwanza ambapo ilikuwa nyuma 58-52, lakini ikaporomoka katika kipindi cha mwisho ilipofungwa 34-2 na kukamilisha mchuano huo 92-54.

Ushirikiano wa Nyakinda na Ariel Okal ulihangaisha Senegal katika robo tatu za kwanza, lakini Wakenya wakazidiwa maarifa kabisa katika robo ya mwisho.

“Hatukucheza robo ya mwisho vizuri,” mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikiri.

Alieleza, “Walikuwa mbele yetu kwa alama sita pekee tukianza robo ya mwisho. Tulikuwa na uchovu. Tulifanya makosa mengi na kuadhibiwa vibaya sana.”

Katika mchuano wa kufunga kazi ya raundi ya kwanza Novemba dhidi ya Msumbiji, Nyakinda alitetemesha kuliko matarajio ya wengi. Alipata fursa yake kubwa katika mchuano huo baada ya Owuor kuondoa Desmond Owili aliyekuwa amepata jeraha.

Nyakinda alichezeshwa dakika 28:02 na kumaliza wa pili katika ufungaji wa alama baada ya kupachika 16. Mkenya mwenzake Tylor Ongwae aliibuka mfungaji bora kwa alama 21.

Nyakinda alikuwa mwiba kutoka mstari wa kufunga penalti alipopachika nne kati ya nne alizopata. Isitoshe, alifunga tatu kati ya nne alama tatu za kutoka nje ya mduara eneo hatari. Pia, alihakikisha amerejesha mipira minne ndani ya kikapu iliyokuwa imegonga ubao ama rimu kabla iharibike. Ushindi huo wa 79-62 umeweka Kenya katika nafasi ya tatu na mwisho ya kuingia AfroBasket nchini Rwanda baadaye mwaka 2020.

Kenya inapatikana nyuma ya viongozi Senegal na nambari mbili Angola nayo Msumbiji inavuta mkia. Timu tatu za kwanza zitafuzu.

  • Tags

You can share this post!

Madiwani wavuna baada ya SRC kuidhinisha kila mmoja apewe...

Bayern wana kiu ya kutwaa Kombe la Dunia kwa Klabu nchini...