• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Afueni kwa West Ham Utd kadi nyekundu ambayo beki Balbuena alionyeshwa dhidi ya Chelsea ikibatilishwa

Afueni kwa West Ham Utd kadi nyekundu ambayo beki Balbuena alionyeshwa dhidi ya Chelsea ikibatilishwa

Na MASHIRIKA

MAAMUZI ya kumwonyesha beki Fabian Balbuena wa West Ham United kadi nyekundu katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha na Chelsea yamebatilishwa.

Hii ni baada ya waajiri wake kufaulu kwenye rufaa waliyokuwa wamewasilisha kwa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kulalamikia maamuzi hayo.

Beki huyo raia wa Uruguay mwenye umri wa miaka 29 alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika dakika ya 81 kwa madai kwamba alimchezea visivyo difenda Ben Chilwell. Chelsea walisajili ushindi wa 1-0 katika gozi hilo lililowapa fursa ya kupaa hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali.

Kwa mujibu wa kocha David Moyes wa West Ham, maamuzi hayo ya kumpa Balbuena kadi nyekundu yalifanywa na mtu ambaye “hajawahi kuingia uwanjani kucheza soka”.

Kubatilishwa kwa maamuzi hayo ni afueni kubwa kwa West Ham na Balbuena ambaye kwa sasa atakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Moyes dhidi ya Burnley kwenye gozi la EPL litakalowakutanisha leo Jumatatu usiku ugani Turf Moor.

Kufikia sasa, West Ham ambao hawajawahi kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL na ni pengo la alama moja pekee ndilo linawatenganisha na nambari tano Tottenham Hotspur. Chelsea wanakamata nafasi ya nne kwa pointi 61.

Huku zikiwa zimesalia mechi tano zaidi kwa kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi, ni matumaini ya Moyes kwamba wapinzani wao wakuu watajikwaa katika michuano ijayo nao washinde mechi zote zilizopo mbele yao na waingie ndani ya orodha ya nne-bora na kufuzu kwa gozi la UEFA msimu ujao.

Hadi refa Chris Kavanagh alipomfurusha Balbuena uwanjani kwa kadi nyekundu, Chelsea walikuwa wakiongoza mchuano huo kwa 1-0 kupitia bao la Timo Werner.

West Ham watawaendea Burnley wakilenga kuendeleza presha kwa Chelsea na Spurs kadri wanavyolenga kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora.

Chini ya kocha Sean Dyche, Burnley watashuka dimbani wakilenga kuimarisha nafasi yao ya kusalia kwenye kivumbi cha EPL muhula huu. Kikosi hicho kwa sasa kinakamata nafasi ya 16 jedwalini kwa pointi 36.

Ni pengo la alama tisa pekee ndilo linawatenganisha Burnley na Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion, wanachungulia hatari ya kuteremshwa ngazi baada ya Sheffield United.

Huku Burnley wakitazamiwa kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Wolves katika mchuano wao uliopita ligini, West Ham watakuwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupepetwa 1-0 na Chelsea wikendi iliyopita.

Nafuu zaidi kwa West Ham ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata kuliko Chelsea waliowapepeta Fulham 2-0 mnamo Jumamosi ugani Stamford Bridge.

Japo West Ham wanapigiwa upatu wa kuzamisha chombo cha Burnley kirahisi, kocha Dyche amekiri kwamba wana kiu ya kujitoa topeni na kufufua makali yao baada ya kutosajili ushindi kutokana na mechi saba zilizopita ugani Turf Moor. Michuano mitano kati ya hiyo ambayo Burnley wamepigia nyumbani ilikamilika kwa sare.

Burnley hawajawahi kutandaza mechi nane za nyumbani bila ushindi tangu 1971 na watapania leo kusajili ushindi wa pili mfululizo kwa mara ya pili muhula huu.

Kuteleza zaidi kwa West Ham waliopoteza mechi mbili zilizopita kwa mfululizo kwa mara ya kwanza tangu Septemba 2020, kutawashuhudia wakishindwa kuhimili presha kali kutoka kwa Liverpool, Tottenham Hotspur na Everton wanaofukuzia pia fursa ya kunogesha soka ya bara Ulaya msimu ujao.

Bao la Michail Antonio liliwavunia West Ham ushindi wa 1-0 dhidi ya Burnley katika mchuano wa mkondo wa kwanza ligini msimu huu ugani London. Hata hivyo, wameshindwa kuwaangusha Burnley mara tatu ugani Turf Moor tangu aliyekuwa kocha wao, Slaven Bilic, awaongoze kusajili ushindi wa 2-1 mnamo Mei 2017.

Katika mchuano mwingine wa leo, West Brom ambao wamejizolea alama 25 kutokana na mechi 33 zilizopita, watakuwa wenyeji wa Wolves wanaokamata nafasi ya 12 kwa alama 41.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Serikali kutumia Sh7 bilioni kununua chanjo ya corona...

Kane na Saka watawazwa Wachezaji Bora wa Mwaka 2021 katika...