• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 2:08 PM
Amonde astaafu kuchezea Kenya Shujaa ikimakiza ya tisa Olimpiki

Amonde astaafu kuchezea Kenya Shujaa ikimakiza ya tisa Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

NAHODHA wa Kenya Shujaa, Andrew Amonde amestaafu kuchezea timu hiyo ya raga ya wachezaji saba kila upande baada ya kuitumikia kwa miaka 15.

Mshambuliaji huyo wa klabu ya KCB alitangaza kustaafu kwake baada ya Shujaa kukamilisha kampeni yake ya Olimpiki 2020 katika nafasi ya tisa kufuatia ushindi wa alama 22-0 dhidi ya Ireland mnamo Julai 28.

Johnstone Olindi, Jacob Ojee, William Ambaka na Daniel Taabu walifunga miguso ya Shujaa dhidi ya Ireland naye Olindi akaongeza mkwaju jijini Tokyo nchini Japan katika mechi hiyo ya kutafuta nambari tisa na 10.

Amonde, ambaye atafikisha umri wake miaka 38 Sikukuu ya Krismasi mwaka huu wa 2021, alifunga mguso mmoja jijini Tokyo katika ushindi wa 21-7 dhidi ya Japan katika nusu-fainali ya nambari tisa hadi 12.

Mwanafunzi huyo wa zamani wa Shule ya Upili ya Kisumu Boys katika kaunti ya Kisumu, alianza uchezaji wa raga ya klabu mwaka 2004 baada ya kukamilisha kidato cha nne.

Alijiunga na Kisumu RFC kabla ya kunyakuliwa na mabwanyenye KCB jijini Nairobi mwaka 2005 ambayo ameichezea maisha yake yote.

Mara yake ya kwanza kuvalia jezi ya Shujaa ilikuwa katika Raga za Dunia za wachezaji saba kila upande mwaka 2006 katika msimu wa 2006-2007 wakati wa duru ya George Sevens nchini Afrika Kusini.

Tangu wakati huo, Amonde, ambaye anafahamika kwa jina la utani kama Opede, amechezea Shujaa katika Kombe la Dunia la raga ya wachezaji saba kila upande mwaka 2013 nchini Urusi na mwaka 2018 nchini Amerika. Kwenye Raga za Dunia, Amonde amesakata michuano 358 na kupachika pointi 320, yote ikiwa ni kupitia miguso 64.

Amonde alikuwa katika kikosi cha kocha marehemu Benjamin Ayimba kilichoandikisha historia kwa kushinda duru kwenye Raga za Dunia wakati Shujaa iliduwaza miamba Fiji 30-7 katika fainali ya Singapore Sevens mwaka 2016. Alikuwa katika kikosi cha kocha kutoka Afrika Kusini Jerome Paarwater kilichokosa pembamba tiketi ya Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande 2015.

Amonde, ambaye alishiriki makala ya kwanza ya Raga za Dunia za wachezaji 10 kila upande nchini Bermuda mwaka 2020, amehitimu na kiwango cha kwanza cha kocha wa mazoezi ya nguvu za kimwili.

 

You can share this post!

Mwili wa mwanamke wapatikana umetupwa kisimani

Wanasoka wa Brazil wafuzu kwa robo-fainali za Olimpiki huku...