• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Andy Murray ajiondoa kwenye tenisi ya mchezaji mmoja kila upande kwa sababu ya jeraha

Andy Murray ajiondoa kwenye tenisi ya mchezaji mmoja kila upande kwa sababu ya jeraha

Na MASHIRIKA

BINGWA mara mbili wa Olimpiki, Andy Murray, 34, amejiondoa kwenye tenisi ya mchezaji mmoja kila upande baada ya kupata jeraha la paja.

Nyota huyo raia wa Scotland aliyeshirikiana na Joe Salisbury kushinda mechi ya wachezaji wawili kila upande mnamo Julai 24, alitarajiwa kumenyana na Felix Auger-Aliassime wa Canada mnamo Julai 26, 2021.

Murray hata hivyo atanogesha tenisi ya wachezaji wawili kila upande baada ya kushauriwa na madaktari kutoshiriki fani zote mbili nchini Japan. Atashirikiana na Salisbury kupepetana na Wajerumani Kevin Krawietz na Tim Puetz katika raundi ya pili. Nafasi yake kwenye tenisi ya mchezaji mmoja kila upande imetwaliwa na Max Purcell wa Australia.

“Yasikitisha kwamba imenilazimu kujiondoa kwenye fani hii baada ya kushauriwa na wataalamu wa afya. Nimekubali maamuzi hayo magumu na lengo langu kwa sasa ni kunyanyua taji la tenisi ya wachezaji wawili kila upande,” akasema Murray.

Kujiondoa kwa Murray na kupigwa kwa Heather Watson katika raundi ya kwanza, sasa kunasaza Liam Broady kuwa mchezaji wa pekee anayewakilisha Uingereza katika tenisi ya mchezaji mmoja kila upande kwenye Olimpiki.

Broady, 27, alifuzu kwa raundi ya pili hapo jana baada ya kumpiku Francisco Cerundolo wa Argentina kwa matokeo ya 5-7, 7-6, 7-4, 6-2. Atakutana na Hubert Hurkacz wa Poland kwenye raundi ya tatu mnamo Julai 26, 2021.

Murray alishinda nishani ya kwanza ya dhahabu katika tenisi ya mchezaji mmoja kila upande kwenye Olimpiki mnamo 2012 jijini London, Uingereza. Alihifadhi ufalme huo miaka minne baadaye jijini Rio de Janeiro, Brazil. Tangu wakati huo, mshindi huyo mara tatu wa Grand Slam amekuwa mwepesi wa kupata mejaraha huku akifanyiwa upasuaji wa paja mara kwa mara.

Ingawa alikosa kipute cha Australian Open mnamo Januari baada ya kuugua Covid-19, alirejea ulingoni kwa matao ya juu na akashinda taji la Wimbledon kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne mnamo Juni 2021.

Kwingineko, mwanatenisi nambari moja duniani, Ashleigh Barty wa Australia aliduwazwa na Sara Sorribes Tormo wa Uhispania kwa kichapo cha 6-4, 6-3 mnamo Julai 25, 2021.

Ushindi huo ndio mnono zaidi kwa Sorribes anayeshikilia nafasi ya 48 duniani kuwahi kusajili kwenye ulingo wa tenisi. Naomi Osaka wa Japan anayeshikilia nafasi ya pili duniani, alimzaba Saisai Zheng wa China 6-1, 6-4.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kenya Shujaa yasalimu amri ya Amerika raga ya wachezaji...

Peaty aweka historia ya kuwa Mwingereza wa kwanza kuhifadhi...