• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Arsenal kwenye mizani ya Sevilla EPL ikinukia

Arsenal kwenye mizani ya Sevilla EPL ikinukia

NA MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

TIMU ya Arsenal itatumai kukamilisha matayarisho ya msimu mpya kwa kishindo itakapopepetana na Sevilla katika Kombe la Emirates ugani Emirates, leo Jumamosi alasiri.

Wanabunduki hao kwa jumla wamekuwa na maandalizi mazuri wanapoelekea kwa mchuano wao wa ufunguzi wa Ligi Kuu (EPL) dhidi ya wenyeji Crystal Palace mnamo Agosti 5.

Walilemea wapinzani Nuremberg 5-3 Julai 8 nchini Ujerumani, na Everton 2-0 Julai 17, Orlando City 3-1 Julai 21 na Chelsea 4-0 Julai 24 nchini Amerika kabla ya kupokea kichapo cha bao 2-1 kutoka kwa Brentford Julai 27 uwanjani London Colney.

Mchuano dhidi ya Seville ni wao wa mwisho kujipiga msasa kabla ya kuvaana na vijana wa kocha Patrick Vieira.

Vijana wengi wameridhisha Arteta akiwemo mshambulizi Eddie Nketiah ambaye ametinga mabao matano. Sajili mpya Gabriel Jesus katika michuano hiyo.

Hata hivyo, kuna wachezaji watatu ambao Arteta atakuwa makini kuwapa fursa dhidi ya Sevilla ikiwezekana.

Kiungo mshambulizi Emile Smith Rowe na mabeki Kieran Tierney na Takehiro Tomiyasu wamejumuika na wenzao mazoezini tangu timu irejee jijini London baada ya kuvurugwa na majeraha, na watatu hao watakuwa makini kupata angaa dakika dhidi ya Sevilla.

Sajili mpya kiungo mshambulizi Fabio Vieira bado anauguza jeraha la mguu naye kipa Bernd Leno anaaminika kukaribia kuyoyomea kwingine.

Jesus na Oleksandr Zinchenko, ambao walitokea Manchester City, wanatarajiwa kucheza ugani Emirates kwa mara ya kwanza. Mabingwa mara sita wa Ligi ya Uropa Sevilla walitoka 1-1 dhidi ya Tottenham Julai 16 kabla ya kulima Sporting Lisbon kwa njia ya penalti 6-5 Julai 24 na kisha kurarua Angers 6-0 Julai 27.

You can share this post!

Utata kuhusu Fomu 34A waondolewa

Sonko sasa aunga Omar wa UDA kuwa gavana

T L