• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Sonko sasa aunga Omar wa UDA kuwa gavana

Sonko sasa aunga Omar wa UDA kuwa gavana

NA WINNIE ATIENO

HATIMAYE aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ameamua kumuunga mkono mgombea wa kiti cha ugavana wa kaunti ya Mombasa kupitia kwa chama cha Naibu wa Rais William Ruto, UDA, Bw Hassan Omar.

Tayari Sonko amejiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na mwaniaji urais wa UDA Dkt William Ruto.

Uamuzi wake unajiri baada ya kupata pigo kubwa Mahakama Kuu ilipotupilia mbali ombi lake la kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumwidhinisha kugombea kiti cha ugavana Mombasa.

“Swali langu ni mgombea wangu mwenza Bw Ali Mbogo alifanya makosa gani? Si wamruhusu agombee ugavana wa Mombasa wakikataa tutamuunga mkono Bw Hassan Omar wa UDA. Lakini nataka kuwaambia wakazi wa Mombasa kuwa uamuzi wa mahakama sio mwisho wa kila kitu,” alisema kwenye mahojiano na runinga ya KTN.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa wanachama wa UDA wakiongozwa na Mbunge wa Nyali Mohammed Ali na mwaniaji wa Ugavana kaunti ya Mombasa, Bw Omar wamekuwa wakimsihi Bw Sonko kujiunga na chama chao huku kesi inayomkabili ikiendelea.

Walisema wako tayari kushirikiana na Bw Sonko ambaye alikuwa Gavana wa Nairobi kabla ya kubanduliwa mwaka 2020, kumaliza uongozi wa Gavana wa Mombasa Bw Hassan Joho na ushawishi wa nduguye mfanyabiashara maarufu Bw Abu Joho.

Bw Sonko alisema hakuenda kwa Uhuru Kenyatta na mgombea wa urais wa Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga ili ‘kusafishwa’.

Hivi majuzi alikutana na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Nataka haki yangu. Kesi dhidi yangu haifai kuhujumu mkuu wa chama chetu cha Wiper Kalonzo Musyoka, Bw Mbogo na watu wangu wa Mombasa. Kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa safari. Ninajua ninapigwa vita na watu wakubwa sana,” alisema.

Bw Omar na Bw Ali walisema wako tayari kuungana na Bw Sonko ambaye alikuwa anawania ugavana kupitia chama cha Wiper akisema wanaweza kushinda uchaguzi huo wa ugavana.

“Tunamkaribisha Bw Sonko huku kwetu,” alisema Bw Ali.

Kiti hicho kinamenyelewa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir (ODM), Bw Omar, Bw Sonko, mfanyabiashara Bw Hezron Awiti (Vibrant Democratic Party), Bw Daniel Kitsao (mgombea huru), Bw Shafii Makazi (UPIA), Bw Said Abdhalla (Usawa Kwa Wote) na naibu gavana wa Mombasa Dkt William Kingi (PAA).

Hata hivyo, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka iliwabandua Bw Sonko na Bw Anthony Chitavi (UDP) kwenye kinyanganyiro hicho.

Bw Sonko aliwasilisha kesi yake mahakamani.

“Nataka kumwambia ndugu yangu Sonko aje tuongee ili tuikomboe Mombasa. Tulikuwa naye katika bunge la seneti tulifanya naye kazi vizuri,” alisema Bw Omar.

Alisema manifesto ya Bw Sonko ya kutaka kumaliza ufisadi na ukabila katika serikali ya kaunti ni sawia na agenda yake.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal kwenye mizani ya Sevilla EPL ikinukia

Karua aahidi ‘kuwakomboa’ wakazi Mlimani

T L