• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Aubameyang astaafu kuichezea timu ya taifa

Aubameyang astaafu kuichezea timu ya taifa

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa Gabon na fowadi wa Barcelona, Pierre-Emerick Aubameyang, 32, amestaafu soka ya kimataifa wiki mbili kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi za mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2023 kupulizwa.

Sogora amechezea Gabon mechi 68 na kufunga mabao 29 yanayomweka kileleni mwa orodha ya wafungaji bora wa muda wote kambini mwa kikosi hicho cha Panthers.

Shirikisho la Soka la Gabon (Fegafoot) limethibitisha kupokea barua ya Aubameyang akitangaza maamuzi hayo ya kuangika daluga zake kimataifa.

“Baada ya miaka 13 ya kuwakilisha taifa langu, ningependa kuwatangazia kwamba nastaafu katika soka ya kimataifa ili nimakinikie zaidi majukumu yangu katika kiwango cha klabu,” akaandika mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Arsenal.

Aubameyang alizaliwa nchini Ufaransa na akawahi kuvalia jezi za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 kabla ya kuhamia kuchezea Gabon kimataifa kwa azma ya kufuata nyayo za baba yake mzazi aliyewahi kuwa nahodha wa Gabon kwenye fainali zao za kwanza za AFCON mnamo 1994.

Aubameyang alifungia Gabon bao katika mechi yake ya kwanza kimataifa na akaongoza kikosi hicho kushinda Morocco 2-1 mnamo 2009 katika mechi ya kufuzu kwa fainali za AFCON. Alikosa kuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Gabon kwenye fainali zilizopita za AFCON baada ya kuambukizwa virusi vya corona akiwa kambini kisha kupatikana na matatizo ya moyo.

Gabon wameratibiwa kuanza kampeni zao za kufuzu kwa AFCON 2023 nchini Ivory Coast kwa kumenyana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ugenini mnamo Juni 4, 2022 kabla ya kualika Mauritania siku nne baadaye katika mechi ya pili ya Kundi I.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Hata akiwania urais huenda Kalonzo asiweze...

Vikao vya bunge vyaongezwa kwa wiki moja zaidi ili...

T L