• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
BADO SWARA! Kenya yaona vimulimuli dhahabu ya mbio za umbali wa mita 10,000 ikisalia ndoto

BADO SWARA! Kenya yaona vimulimuli dhahabu ya mbio za umbali wa mita 10,000 ikisalia ndoto

Na MASHIRIKA

TOKYO, Japan

KENYA iliondoka kavukavu katika mbio za wanaume za mita 10,000 kwenye mashindano ya Olimpiki hapo jana, baada ya Rodgers Kwemoi, Rhonex Kipruto na Weldon Langat kusikitisha nchini Japan.

Ukame huo wa miaka 52, miezi tisa na siku 18 utaendelea kuwa kizungumkuti kwa taifa, hususan baada ya Shirikisho la Riadha nchini (AK) kuwa na matumaini ya kupunga pepo huyo katika Olimpiki za mwaka huu.

Kwemoi alionyesha dalili kwamba anaweza kufuata nyayo za Naftali Temu, aliyeshindia Kenya dhahabu katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara 25 kwenye Olimpiki 1968.

Alichupa uongozini ikisalia mizunguko minne jijini Tokyo, lakini hakuwa na lake baada ya kengele ya mzunguko wa mwisho kulia.

Mkenya mwenzake, Kipruto – ambaye aliingia timuni baada ya mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia ya kilomita 21, Geoffrey Kamworor, kuumia kifundo akiwa mazoezini – aliongoza kidogo mizunguko hiyo 25.

Kisha, uongozi ukaendea bingwa wa dunia na mshikilizi wa rekodi ya dunia Joshua Cheptegei kutoka Uganda, kabla Kwemoi kuamua kwenda mbele.

Hata hivyo, alijipata amefungiwa njia kisha akapitwa na raia wa Canada Mohammed Ahmed, kabla Selemon Barega wa Ethiopia kuchomoka na kuwaacha wapinzani wenzake bila jibu.

Barega alishinda taji hilo kwa dakika 27:43.22 akirejeshea taifa lake ubingwa ambao ilishinda mara nne kati ya 1996 na 2008, kabla Muingereza mwenye asili ya Somalia, Mo Farah, kutawala 2012 na 2016.

Cheptegei aliridhika na nafasi ya pili (27:43.63) naye Kiplimo (27:43.88) akafunga mduara wa tatu-bora wa kupokea medali.

Kwemoi alirushwa hadi nambari saba naye Kipruto akakamata nafasi ya tisa. Langat alimaliza katika nafasi ya 20 kati ya watimkaji 25 walioshiriki fainali hiyo.

Licha ya ukame wa dhahabu tangu 1968, Kenya imekuwa ikijikakamua kupata medali katika mbio hizo; ya hivi punde ikiwa nishani ya fedha kupitia kwa Paul Tanui katika Olimpiki za 2016 jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Matokeo (10-bora): Selemon Barega (Ethiopia) dakika 27:43.22, Joshua Cheptegei (Uganda) 27:43.63, Jacob Kiplimo (Uganda) 27:43.88, Berihu Aregawi 27:46.16, Grant Fisher (Amerika) 27:46.39, Mohammed Ahmed (Canada) 27:47.76, Rodgers Kwemoi (Kenya) 27:50.06, Yomif Kejelcha (Ethiopia) 27:52.03, Rhonex Kipruto (Kenya) 27:52.78, Morhad Amdouni (Ufaransa) 27:53.58.

You can share this post!

Klabu za Barcelona, Juventus na Real Madrid zaendelea...

Obiri kuongoza Kenya kuhifadhi dhahabu ya Olimpiki mita...