• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Obiri kuongoza Kenya kuhifadhi dhahabu ya Olimpiki mita 5,000

Obiri kuongoza Kenya kuhifadhi dhahabu ya Olimpiki mita 5,000

Na MASHIRIKA

WAKENYA Hellen Onsando Obiri, Agnes Jebet Tirop na Lilian Rengeruk Kasait jana waliweka hai matumaini ya Kenya kuhifadhi dhahabu ya Olimpiki, kwenye fainali ya mbio za mita 5,000 za wanawake mnamo Jumatatu jijini Tokyo, Japan.

Kasait, aliyeshinda mbio za nyika duniani mnamo 2017, alikuwa wa mwisho kufuzu kutoka kundi la kwanza la mchujo lililojumuisha pia Tirop na bingwa wa dunia katika 10,000m na 1,500m, Sifan Hassan wa Uholanzi.

Bingwa huyo wa Afrika 2018 aliambulia nafasi ya tano kwa muda wa dakika 14:50.36, nyuma ya Waethiopia Teferi Senbere (14:48.31) na Taye Ejgayehu (14:48.52).

Mchujo huo ulitawaliwa na Hassan (14:47.89) huku Tirop, aliyezoa nishani ya shaba katika 10,000m kwenye Riadha za Dunia za 2017 na 2019, akiridhika na nafasi ya pili (14:48.01).

Obiri, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya kitaifa (14:18.37), alimaliza nambari mbili katika mchujo wa pili kwa dakika 14:55.77.

Bingwa huyo mara mbili wa dunia katika 5,000m (2017 na 2019), alizidiwa ujanja na Tsegay Gudaf wa Ethiopia (14:55.74) aliyetamalaki kivumbi hicho cha mizunguko 12 na nusu kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Nadia Battocletti (Italia), Elise Cranny (Amerika) na Karoline Bjerkeli (Norway) pia walifuzu.

You can share this post!

BADO SWARA! Kenya yaona vimulimuli dhahabu ya mbio za...

FUNGUKA: ‘Haja yangu pesa tu!’