• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:02 AM
Bamford aongoza Leeds United kuaibisha Crystal Palace kwenye gozi la EPL

Bamford aongoza Leeds United kuaibisha Crystal Palace kwenye gozi la EPL

Na MASHIRIKA

FOWADI Patrick Bamford alifunga bao lake la 100 na kuwaongoza waajiri wake Leeds United kuwapepeta Crystal Palace 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatatu usiku uwanjani Elland Road.

Ushindi huo uliwapaisha Leeds United wanaonolewa na kocha Marcelo Bielsa hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 32, moja kuliko Arsenal ambao wamesakata mechi moja zaidi.

Bamford, 27, alifunga bao la pili la Leeds United katika dakika ya 52 baada ya kipa Vicente Guaita wa Palace kutema kombora aliloelekezewa na Raphinha.

Leeds walijiweka uongozini katika mechi hiyo mapema kupitia bao la dakika ya tatu lililojazwa kimiani na Jack Harrison aliyemzidi ujanja beki Gary Cahill.

Mabao 100 ambayo sasa yanajivuniwa na Bamford yanajumuisha 21 aliyofunga wakati akichezea MK Dons kwa mkopo, manane akivalia jezi za Derby, 33 akiwasakatia Middlebrough na 38 akiwa fowadi wa Leeds United.

“Muhimu zaidi katika mechi iliyotukutanisha na Palace ilikuwa ni kutia kapuni alama tatu. Sikutarajia kwamba mechi hiyo ingenipa jukwaa la kufikisha jumla ya mabao 100 kitaaluma,” akasema Bamford aliyewahi kuchezea Chelsea kwa miaka mitano kabla ya kuchezea vikosi vingine saba kwa mkopo.

Kushindwa kwa Palace kuliwashusha hadi nafasi ya 13 kwa alama 29 sawa na Southampton.

Bamford kwa sasa anajivunia mabao 12 kufikia sasa katika EPL msimu huu na ni wanasoka wawili pekee raia wa Uingereza wanaomzidi kwa idadi ya mabao – Harry Kane wa Tottenham Hotspur na Dominic Calvert-Lewin wa Everton ambao wamefunga mabao 13 kila mmoja.

Makali ya Bamford kufikia sasa yanatarajiwa kumpa nafasi katika timu ya taifa ya Uingereza inayojiandaa kwa mechi tatu za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 mwishoni mwa Machi – dhidi ya San Marino na Poland ugenini kisha Albania nyumbani.

Leeds United kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Arsenal katika mechi ya EPL mnamo Februari 14 huku Crystal Palace wakialika Burnley uwanjani Selhurst Park mnamo Februari 13, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Man-City na Liverpool kucheza mechi zao za UEFA dhidi ya...

Omanga asema haendi popote