• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Barcelona watandika Real Madrid na kutawazwa wafalme wa Spanish Super Cup

Barcelona watandika Real Madrid na kutawazwa wafalme wa Spanish Super Cup

Na MASHIRIKA

KOCHA Xavi Hernandez alinyanyua taji lake la kwanza akidhibiti mikoba ya Barcelona kufuatia ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na masogora wake dhidi ya Real Madrid kwenye fainali ya Spanish Super Cup mnamo Jumapili nchini Saudi Arabia.

Barcelona wanaoongoza jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) walitamalaki mechi kuanzia dakika ya kwanza na wakawekwa kifua mbele na chipukizi Pablo Gavira, 18, baada ya kushirikiana vilivyo na kigogo Robert Lewandowski.

Lewandowski alipachika wavuni bao la pili la Barcelona baada ya kumegewa krosi na Gavi ambaye pia alichangia bao lililofumwa wavuni na Pedro Lopez. Karim Benzema alifuta machozi ya Real mwishoni mwa kipindi cha pili.

Barcelona wangalifunga mabao zaidi ila kipa Thibaut Courtois akajituma zaidi na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na wavamizi wa Barcelona wakiwemo Ousmane Dembele na Lewandowski aliyeshutia mojawapo ya fataki zake zikibusu mhimili wa goli.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu 2018 kwa Barcelona kutawazwa wafalme wa Super Cup.

Gavira alivunja rekodi ya kocha wake wa sasa, Xavi, na  kuwa mfungaji mchanga zaidi katika historia ya fainali ya Spanish Super Cup.

Barcelona waliwahi kukutana na Real kwenye La Liga mnamo Oktoba 2022 na wakakomolewa 3-1 katika pambano hilo la El Clasico ugani Bernabeu.

Tangu wakati huo, Barcelona walijinyanyua upesi na sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la La Liga kwa alama 41, tatu zaidi kuliko mabingwa watetezi Real wanaokamata nafasi ya pili. Ushindi dhidi ya Real mnamo Jumapili uliendeleza rekodi ya kutopigwa kwa Barcelona katika mechi tisa zilizopita katika mapambano yote.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ruto akana kumwekea mtego Gachagua

Benjamin Tayari ateuliwa mwenyekiti mpya wa bodi ya KPA

T L