• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Bayern Munich wacharaza Dortmund na kutwaa taji la Bundesliga kwa mara ya 10 mfululizo

Bayern Munich wacharaza Dortmund na kutwaa taji la Bundesliga kwa mara ya 10 mfululizo

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya 10 mfululizo baada ya kutandika watani wao wakuu Borussia Dortmund 3-1 mnamo Jumamosi uwanjani Allianz Arena.

Chini ya kocha Julian Nagelsmann, Bayern waliwatamalaki Dortmund kwa mara nyingine msimu huu na ushindi uliwawezesha kufungua mwanya wa alama 12 kati yao na Dortmund kileleni mwa jedwali la Bundesliga zikisalia mechi tatu pekee msimu huu.

Nyota wa zamani wa Arsenal, Serge Gnabry, aliwafungulia Bayern ukurasa wa mabao katika dakika ya 15 kabla ya kigogo Robert Lewandowski kufunga goli la pili katika dakika ya 34.

Ingawa penalti ya Emre Can ilirejesha Dortmund mchezoni mwanzoni mwa kipindi cha pili, Jamal Musiala wa Bayern alizamisha kabisa chombo cha wageni wao dakika saba kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Musiala, 19, alivurumisha kombora hatua chache kutoka eneo la penalti na kusisimua mashabiki wa Bayern waliosherehekea ushindi wa kikosi chao kwa mbwembwe za kila sampuli. Taji la Bayern lilikuwa lao la 32 katika Bundesliga.

Ushindi wa Bayern unajiri wakati ambapo kocha Nagelsmann amekiri kupokea jumbe za kumtishia maisha mitandaoni tangu waajiri wake wabanduliwe na Villarreal ya Uhispania kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Licha ya kushindwa kuendeleza makali yaliyowazolea taji la UEFA mnamo 2019-20 baada ya kukomoa Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa mnamo 2019-10 nchini Ufaransa, Bayern hawajashikika katika soka ya Bundesliga.

Fowadi Thomas Muller ambaye sasa ni mchezaji wa kwanza kuwahi kushinda mataji 11 ya Bundesliga, alisema: “Imekuwa fursa ya kuweka rekodi wazi. Sasa kila kitu kiko shwari na ushindi umekuwa wa kuridhisha.”

Ushindi wa Bayern uliendeleza rekodi yao ya kutoshindwa katika mechi tisa mfululizo huku wakipoteza michuano minne pekee ligini kufikia sasa muhula huu.

Lewandowski amefungia Bayern mabao 33 muhula huu baada ya kuweka rekodi ya kupachika wavuni magoli 41 msimu uliopita wa 2020-21.

Mustakabali wa Lewandowski kambini mwa Bayern bado haujulikani ikizingatiwa kwamba mkataba wake wa sasa ugani Allianz Arena utakatika rasmi mnamo 2023. Dortmund pia huenda pia wakalazimika kusajili fowadi mpya kwa kuwa tegemeo lao Erling Braut Haaland anatarajiwa kuyoyomea Uingereza kuvalia jezi za Manchester City.

Haaland ambaye ni raia wa Norway mwenye umri wa miaka 21 amefungia Dortmund jumla ya mabao 21 katika Bundesliga kutokana na mechi 21 msimu huu.

Bayern wameshinda mataji yao matano yaliyopita ya Bundesliga kwa jumla ya alama 64, ufanisi unaodhihirisha ukubwa wa kiwango cha uthabiti wa kikosi chao.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumamosi):

Bayern 3-1 Dortmund

Cologne 3-1 Arminia

Frankfurt 2-2 Hoffenheim

RB Leipzig 2-1 Union Berlin

Freiburg 3-1 M’gladbach

Furth 1-4 Leverkusen

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

441 kukosa matokeo ya KCSE sababu ya udanganyifu

Alfred Keter kuhama UDA, kuwa mgombea huru Nandi Hills

T L