• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Benzema aongoza Real Madrid kukomoa Eintracht Frankfurt na kuzoa taji la Uefa Super Cup

Benzema aongoza Real Madrid kukomoa Eintracht Frankfurt na kuzoa taji la Uefa Super Cup

Na MASHIRIKA

KARIM Benzema aliweka hai matumaini ya kuibuka mshindi wa taji la Ballon d’Or mwaka huu baada ya kufunga bao lake la 324 ndani ya jezi za Real Madrid waliokomoa Eintracht Frankfurt 2-0 mnamo Jumatano na kuzoa ufalme wa Uefa Super Cup jijini Helsinki, Finland.

Real wanaonolewa na kocha Carlo Ancelotti walifuzu kwa kipute cha Super Cup baada ya kutandika Liverpool 1-0 na kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mwishoni mwa msimu wa 2021-22.

Miamba hao wa soka ya Uhispania waliwekwa kifua mbele na beki David Alaba aliyemwacha hoi kipa Kevin Trapp baada ya kujaza kimiani krosi ya Casemiro katika dakika ya 37.

Benzema alifunga bao la pili la Real kunako dakika ya 65 baada ya kushirikiana vilivyo na Vinicius Jr. Bao hilo la Benzema lilimwezesha kumpita kigogo Raul Gonzalez na kumkaribia Cristiano Ronaldo katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote kambini mwa Real. Ronaldo aliwahi kupachika wavuni magoli 450 akivalia jezi za Real kabla ya kuyoyomea Juventus kisha Manchester United.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Frankfurt ambao ni washikilizi wa taji la Europa League kunogesha kipute cha Super Cup. Kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kilipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Daichi Kamada.

Benzema, 34, alishuka dimbani dhidi ya Frankfurt akijivunia kupachika wavuni mabao 44 kutokana na mechi 46 katika mapambano ya msimu wa 2021-22 yaliyoshuhudia Real wakitia kibindoni mataji ya UEFA na Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Mara ya mwisho kwa Real kuvaana na Frankfurt ilikuwa 1960 ambapo miamba hao wa Uhispania walivuna ushindi wa 7-3 katika fainali ya European Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Mchakato wa kumchagua gavana Mombasa...

Timo Werner arejea kambini mwa RB Leipzig baada ya kuagana...

T L