• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Brazil na Ivory Coast nguvu sawa kwenye Olimpiki

Brazil na Ivory Coast nguvu sawa kwenye Olimpiki

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Olimpiki, Brazil, walilazimishiwa sare tasa na Ivory Coast kwenye mchuano wa Kundi D mnamo Jumapili jijini Yokohama, Japan.

Chini ya kocha Andre Jardine, Brazil walitandaza mchuano huo dhidi ya Ivory Coast kwa zaidi ya dakika 80 wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya beki Douglas Luiz wa Aston Villa kuonyeshwa kadi nyekundu.

Japo Luiz, kwenye tukio la kumchezea vibaya fowadi Max Gradel, alionyeshwa kadi ya manjano, refa alibatilisha maamuzi hayo haraka baada ya kurejelewa na teknolojia ya VAR hivyo akamuonyesha kadi nyekundu.

Ivory Coast pia kwa upande wao walikamilisha mechi hiyo na wachezaji 10 uwanjani baada ya kiungo Eboue Kouassi kufurushwa kwa kadi mbili za manjano mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kouassi na Luiz sasa watakosa mechi za mwisho zitakazosakatwa na vikosi vyao katika Kundi D.

Brazil ambao sasa wanaoongoza Kundi D, waliteremka uwanjani wakipigiwa upatu wa kukandamiza Ivory Coast baada ya kusajili ushindi wa 4-2 dhidi ya Ujerumani katika mchuano wa kwanza kundini. Brazil wako chini ya nahodha Dani Alves, 38, ambaye ni sogora mkongwe zaidi kwenye kampeni za Olimpiki 2020 zinazoandaliwa mwaka 2021.

Ivory Coast ya mkufunzi Haidara Soualiho iliwatandika Saudi Arabia 2-1 katika gozi la awali lililowakutanisha Julai 22, 2021.

Katika kipindi cha miaka 45 iliyopita, Brazil wameshindwa kuzoa medali ya Olimpiki mara moja pekee. Kikosi hicho sasa kimeshinda mechi tatu kati ya nne zilizopita na kupachika wavuni mabao 12.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

GUMZO: Wanasema Werner amechoka kusugua benchi ya Chelsea

Ufaransa wazima ndoto ya Afrika Kusini kwenye Olimpiki