• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Ufaransa wazima ndoto ya Afrika Kusini kwenye Olimpiki

Ufaransa wazima ndoto ya Afrika Kusini kwenye Olimpiki

Na MASHIRIKA

ANDRE-PIERRE Gignac alifunga mabao matatu katika kipindi cha pili na kusaidia Ufaransa kutoka nyuma mara tatu kabla ya kupepeta Afrika Kusini 4-3 katika ushindi ulioweka hai matumaini yao ya kushinda nishani kwenye Olimpiki.

Baada ya kupoteza mchuano wao wa kwanza katika Kundi A, dalili zote ziliashiria kwamba Ufaransa wangaliaga Olimpiki za Tokyo, Japan.

Hata hivyo, Gignac ambaye ni fowadi wa zamani wa Olympique Marseille nchini Ufaransa, alisawazisha mambo kupitia penalti katika dakika ya 85 kabla ya Teji Savanier kufungia Ufaransa bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

SGignac ambaye huvalia jezi za Tigres nchini Mexico, ndiye mfungaji bora kwenye Olimpiki za Tokyo kufikia sasa baada ya kupachika wavuni mabao manne kutokana na michuano miwili.

Afrika Kusini ambao matumaini yao ya kusonga mbele kwenye Olimpiki yamezimika, walifunga mabao yao dhidi ya Ufaransa kupitia Kobamelo Kodisang, Evidence Makgopa na Teboho Mokoena.

Chini ya kocha David Notoane, Afrika Kusini walishuka dimbani wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 na Japan kwenye mchuano wa kwanza wa Kundi A.

Ufaransa walijitosa ulingoni wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupigwa 4-1 na Mexico mnamo Julai 22, 2021.

Vijana hao wa kocha Sylvain Ripoll wanapigiwa upatu wa kutwaa dhahabu ya Olimpiki mwaka huu baada ya kushindwa kutinga fainali ya Euro 2019 na 2021 miongoni mwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21.

Dhahabu ya pekee ambayo Ufaransa wanajivunia kwenye Olimpiki ni ile waliyojizolea mnamo 1984. Tangu wakati huo, wametinga fainali ya mashindano hayo mara moja pekee ambapo ni 1996.

Afrika Kusini watachuana na Mexico katika mchuano ujao huku Ufaransa wakipimana ubabe na wenyeji Japan mnamo Julai 28, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Brazil na Ivory Coast nguvu sawa kwenye Olimpiki

Wanawake saba wakamatwa kwa kutengeneza pombe haramu kwenye...