• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Cameroon wakomoa Gambia na kuingia nusu-fainali ya AFCON

Cameroon wakomoa Gambia na kuingia nusu-fainali ya AFCON

Na MASHIRIKA

KARL Toko Ekambi alifunga mabao mawili katika kipindi cha pili na kusaidia wenyeji Cameroon kufuzu kwa nusu-fainali za Kombe la Afrika (AFCON) baada ya kudengua Gambia mnamo Jumamosi usiku.

Toko Ekambi aliwaweka Cameroon kifua mbele katika dakika ya 50 baada ya kukamilisha krosi ya Collins Fai. Alipachika wavuni bao la pili katika dakika ya 57 baada ya kupokezwa pasi safi kutoka kwa Martin Hongla.

Cameroon sasa watavaana na mshindi wa robo-fainali nyingine kati ya Misri na Morocco mnamo Februari 3 kabla ya fainali kuandaliwa Februari 6, 2022.

Gambia walikuwa wakinogesha fainali za AFCON kwa mara ya kwanza muhula huu na walisonga mbele kutoka hatua ya makundi baada ya kutandika Mauritania na Tunisia kabla ya kudengua Guinea katika raundi ya 16-bora.

Cameroon wangalifunga mabao zaidi katika kipindi cha pili katika uwanja wa Japoma jijini Douala kupitia kwa Fai na Vincent Aboubakar ambaye sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora wa kipute cha AFCON mwaka huu kwa magoli sita.

Toko Ekambi sasa ana mabao matano na ushirikiano mkubwa kati yake na Aboubakar unapigiwa upatu kuvunia Cameroon taji la sita la AFCON mwaka huu.

Cameroon walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo kwa mara ya kwanza tangu mashabiki wanane wage dunia baada ya mkanyagano kushuhudiwa nje ya uwanja wa Olembe jijini Yaounde kabla ya kupigwa kwa mechi iliyowakutanisha na Comoros katika hatua ya 16-bora mnamo Januari 24, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AFCON: Burkina Faso wang’oa Tunisia kwenye...

Ruto hatarini kwa ‘kubagua’ vyama vidogo Mlima Kenya

T L