• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Cavani sasa kuchezea Manchester United hadi Juni 2022

Cavani sasa kuchezea Manchester United hadi Juni 2022

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer amefichua kwamba mshambuliaji Edinson Cavani, 34, atakuwa radhi kuongeza mwaka mmoja mwingine kambini mwa Manchester United baada ya mkataba mpya ambao ameutia saini ugani Old Trafford kutamatika Juni 2022.

Sogora huyo raia wa Uruguay amefufua makali yake mwishoni mwa msimu huu ambapo amepachika wavuni jumla ya mabao manane kutokana na mechi saba zilizopita.

Sasa ataendelea kuhudumu uwanjani Old Trafford, Uingereza hadi Juni 2022 kabla ya kuamua iwapo ataendelea kuchezea Man-United au atahamia Argentina kuvalia jezi za kikosi cha Boca Juniors.

“Nimejenga uhusiano mzuri na klabu hii na najihisi kuwa sehemu ya historia ndefu ya mafanikio yake. Ninajivunia mlahaka mzuri na wachezaji wenzangu pamoja na wafanyakazi wote wengine wanaokihangaikia kikosi hiki nyuma ya pazia,” akasema Cavani.

Cavani ambaye hakuwa ameamua kuongeza kandarasi yake kwa mwaka mmoja zaidi au kutua kambini mwa Boca Juniors, aliongeza kwamba: “Man-United wananipa msukumo wa kujitahidi uwanjani mara kwa mara. Nina imani kwamba kufaulu zaidi na kuwapa mashabiki wetu kitu spesheli pamoja na kuvunia timu mataji ya haiba msimu ujao.”

Tangu ajiunge na Man-United bila ada yoyote mnamo Oktoba 2020, Cavani ambaye ni sogora wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG), amefungia mabingwa hao mara 20 wa taji la EPL jumla ya mabao 15 kutokana na mapambano yote. Bao lake la mwisho kambini mwa kikosi hicho ni katika ushindi wa 3-1 waliousajili dhidi ya Aston Villa katika EPL mnamo Mei 9, 2021.

Cavani amekuwa miongoni mwa wavamizi wakuu katika soka ya bara Ulaya kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 iliyopita. Alifungia PSG jumla ya magoli 200 kutokana na mechi 301 alizopigia miamba hao wa soka ya Ufaransa tangu alipoagana rasmi na Napoli ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Kikubwa zaidi kilichomchochea kuagana na PSG mnamo 2020 ni wingi wa mizozo kati yake na mshambulia mahiri raia wa Brazil, Neymar Jr.

“Nilisema kwamba ujio wa Cavani ungeleta nguvu mpya na motisha zaidi kikosini. Sote tumeona hilo likifanyika. Tunamhitaji kwa msimu mmoja zaidi atufikishe tunakolenga kufika muhula ujao wa 2021-22,” akasema kocha wa Man-United, Ole Gunnar Solskjaer.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Malalamiko ya ODM uchaguzi mdogo Bonchari

Ahmed Ali Muktar ndiye Gavana mpya wa Wajir