• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Jorginho afunga penalti mbili na kusaidia Chelsea kuzamisha Aston Villa ligini

Jorginho afunga penalti mbili na kusaidia Chelsea kuzamisha Aston Villa ligini

Na MASHIRIKA

JORGINHO alifunga penalti mbili na kusaidia Chelsea kutoka chini kwa bao moja na kutandika Aston Villa 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili usiku.

Ushindi huo ulidumisha Chelsea katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 41 sawa na Liverpool ambao wana mechi moja zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya michuano ambayo imesakatwa na washindani wao wakuu wakiwemo viongozi na mabingwa watetezi Manchester City.

Villa walijiweka uongozini katika dakika ya 28 kupitia bao la beki Reece James aliyejifunga baada ya kuzidiwa ujanja na mpira kutoka kwa Matt Targett.

Hata hivyo, Chelsea walisawazisha dakika sita baadaye kupitia kwa Jorginho aliyefunga penalti iliyotokana na tukio la Callum Hudson-Odoi kuchezewa visivyo na Matty Cash ndani ya kijisanduku.

Mvamizi Romelu Lukaku aliyekuwa amekosa mechi tatu mfululizo kutokana na Covid-19, aliingizwa ugani mwanzoni mwa kipindi cha pili na akafunga bao baada ya dakika 11 kutokana na krosi ya Hudson-Odoi.

Lukaku alichangia pia bao la tatu la Chelsea ambalo Jorginho alipachika wavuni kupitia penalti mwishoni mwa kipindi cha pili. Bao hilo la Jorginho lilikuwa lake la tisa msimu huu na la sita kutokana na michuano sita ya EPL.

Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Chelsea kusajili ligini baada ya mechi tatu. Sasa ni pengo la alama sita ndilo linatamalaki kati yao na Man-City waliopepeta Leicester 6-3 ugani Etihad.

Chelsea walikuwa kileleni mwa jedwali la EPL baada ya kushinda Watford 2-1 mnamo Disemba 1, 2021. Hata hivyo, alama tano walizojizolea kutokana na mechi nne ziliwateremsha jedwalini hadi wakajipata chini ya Man-City na Liverpool ambao pia ni miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la EPL muhula huu.

Villa walisakata mechi hiyo dhidi ya Chelsea bila kocha Steven Gerrard aliyepatikana na virusi vya corona. Nafasi ya Gerrard ambaye ni kiungo na nahodha wa zamani wa Liverpool ilitwaliwa na msaidizi wake, Gary McAllister.

Chelsea ni miongoni mwa vikosi vya EPL ambavyo vimeathiriwa pakubwa na maambukizi mapya ya virusi vya corona. Hata hivyo, ombi la kocha Thomas Tuchel kutaka mchuano uliokutanisha kikosi chake na Wolves uwanjani Molineux mnamo Disemba 19 kuahirishwa, liligonga mwamba.

Mabingwa hao wa EPL 2016-17 walikuwa bila wanasoka Kai Havertz na Timo Werner japo walikaribisha kikosi fowadi Lukaku na kiungo mvamizi Hudson-Odoi.

Villa kwa sasa wanakamata nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 22 sawa na Leicester City ya kocha Brendan Rodgers.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

OKA kumtaja mwaniaji wa urais Januari

Kanisa lakosoa chanjo ya lazima

T L